IQNA

Shakhsia Katika Qur'ani /15

Nabii Lut; Miaka 20 ya istikama na kusimama kidete dhidi ya Wenye Dhambi

16:59 - November 15, 2022
Habari ID: 3476093
TEHRAN (IQNA) – Nabii Lut- Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-(AS)- alikuwa miongoni mwa masahaba wa Nabii Ibrahim (AS) katika kuwalingania watu kwenye Tauhidi au imani Mungu Mmoja. Alipewa jukumu la kusafiri katika miji mingine ili kukuza Tauhidi

Katika njia hii, alikabiliwa na matatizo na manyanyaso mengi lakini kwa namna ya kupongezwa alibaki mvumilivu na dhabiti na aliendelea na juhudi zake za kuwaongoza watu.

Lut alikuwa mwana wa Harani na mjukuu wa Tarokh. Jina lake limetajwa katika Qur'ani Tukufu mara 27. Qur'ani Tukufu inamtaja kuwa ni nabii wa Mwenyezi Mungu na mtu mwadilifu ambaye alikabiliana na watu waliomdunisha na wenye dhambi. Aliwaita watu hawa kwenye dini ya Ibrahim (AS) lakini wakamuasi.

Nabii Lut (AS) alikuwa jamaa yake Nabii Ibrahim (AS). Kulingana na maelezo tofauti alikuwa binamu, mpwa wa Ibrahim (AS), au shemeji yake. Baada ya Ibrahim (AS) kuanza mwaliko wake, Lut (AS) alikubali imani na akafuatana na Ibrahim (AS) kwenye ardhi ya Kanaan (Palestina). Baadaye, aliagizwa na Mwenyezi Mungu kwenda katika miji na ardhi nyingine, hasa ardhi ya Mutfikat, kuwaalika watu kwenye njia iliyonyooka.

Watu wa Mutfikat walifanya madhambi kama vile kulawiti. Mutfikat ni miongoni mwa ardhi ambazo watu wake walipata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa Qur'ani.

Kitabu kitakatifu kinasema watu walifanya ulawiti, ujambazi na kuwanyanyasa wageni wao. Lut (AS) aliwaalika kuikubali dini ya Ibrahim (AS) lakini wao walikataa na kumsumbua.

Lut (AS) alifanya juhudi kwa miaka 20 kuwaongoza kwenye njia iliyonyooka lakini walisisitiza juu ya dhambi zao na hatimaye wakaadhibiwa na Mungu.

Qur'ani inataja jina la Lut (AS) mara 27 na inamrejelea kwa sifa kama vile Hikma  na elimu. Katika vyanzo vingine, ameelezewa na sifa kama ukarimu na mwenye kuwakirimu wageni.

Mkewe amesawiriwa kama mhusika hasi. Alitetea madhambi yaliyotendwa na watu na hata kuwasaidia kumsumbua Lut (AS). Kwa mujibu wa aya za Qur'ani na maelezo ya kihistoria, aliadhibiwa na Mwenyezi Mungu kama watu wengine wa Mutfikat.

Lut (AS) alikuwa na mabinti wawili, mmoja wao akiwa mama yake Nabii Ayyub (Ayubu). Nabii Shuayb (AS) pia ametajwa kuwa ni mkwe wa Lut (AS). Mabinti wa Lut (AS) waliondoka mjini pamoja naye kabla ya kuja kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya hadithi kuhusu Lut (AS) na watu wake, ikiwa ni pamoja na kuja Malaika katika mji wa Sodoma, kuadhibiwa kwa watu, na Lut (AS) na mabinti zake kuokolewa na adhabu, zimetajwa katika Taurati.

Nabii Lut (AS) inasemekana alizikwa katika mji wa Bani Naeem katika mkoa wa Al-Khalil wa Palestina sasa.

captcha