IQNA

Shakhsia Katika Qur’ani /17

Is’haq; Baba wa Manabii wa Bani Israil

22:13 - November 27, 2022
Habari ID: 3476157
TEHRAN (IQNA) – Is’haq alikuwa mtoto wa pili wa Nabii Ibrahim (AS). Is’haq (AS) alikuja kuwa mtume baada ya kaka yake Ismail (AS).

Is’haq (AS) ni babu wa Mitume wa Bani Isra’il. Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Is’haq (AS) alikuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim na Sarah, mama yake.

Is’haq (AS) alizaliwa Palestina na aliishi huko. Alizaliwa miaka 5 au 13 baada ya Ismail (AS), kulingana na baadhi ya riwaya. Alipozaliwa, Ibrahim (AS) alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 100 na Sarah alikuwa na zaidi ya miaka 90.

Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu aliwapa Ibrahim (AS na Sarah habari za kuzaliwa Is’haq (AS). “Na mkewe alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukambashiria (kuzaliwa) Is’haq, na baada ya Is-haq Yaaqub” (Surah Hud, Aya ya 71)

Baada ya kaka yake Ismail (AS) kufariki, Is’haq (AS) alimrithi kuwa mtume na mitume wengine wote wa Mwenyezi Mungu ni kutoka katika kizazi chake, isipokuwa Mtume Muhammad (SAW) ambaye ni dhuria wa Ismail (AS).

Aya nane za Qur’ani Tukufu moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja zinaashiria utume wa Is’haq (AS) na kwa kuzingatia aya hizi, aliendeleza dini ya baba yake ambayo msingi wake ulikuwa ni Tauhidi.

Hakuna dalili kuwa alipokea kitabu kitakatifu. Miongoni mwa sifa zinazonasibishwa na Is’haq (AS) ndani ya Qur’an ni kuwa mfuasi wa Tauhidi , kuwa mwadilifu, kuwa Imamu, mwenye  Ikhlasi (usafi wa nia), kuwa na nguvu na kuwa na utambuzi au uono wa mbali..

Katika Agano la Kale, inasemekana kwamba Is’haq alikuwa mtoto ambaye Ibrahim (AS) alikuwa anakwenda kumtoa dhabihu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Akiwa na umri wa miaka 40, Is’haq (AS) alioa msichana aliyeitwa Rafaqa na kupata watoto wawili wa kiume walioitwa Ais na Yaquub. Kabla ya kifo chake, Is’haq (AS), alimteua Yaquub kama Nabii kufuatia amri ya Mwenyezi Mungu,

Kwa mujibu wa Kitabu cha Mwanzo katika Agano la Kale, Is’haq (AS) mwishoni mwa maisha yake, alipokuwa mzee na kipofu, alifikiria kumtambulisha mmoja wa wanawe kama Wasi (wasii wake). Baada ya hapo Is’haq (AS) aliishi miaka 20 zaidi na kisha akafa akiwa na umri wa miaka 180 huko Al-Khalil (Hebron).

Baadhi ya wafasiri na wanahistoria wa Qur’ani wanaamini kwamba Is’haq (AS) aliishi miaka 160 na baada ya kifo alizikwa Al-Khalil.

captcha