IQNA

Jinai ya magaidi

Magaidi wa Daesh waia raia 53 katika hujuma nchini Syria

13:51 - February 18, 2023
Habari ID: 3476579
TEHRAN (IQNA)- Raia wasiopungua 53 wameuawa katika shambulio linaloaminika kufanywa na magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika mkoa wa Homs, magharibi mwa Syria.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, miili ya wahanga hao imepelekwa katika hospitali ya serikali ya mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs.

SANA imeeleza katika ripoti yake hiyo kuwa, raia hao walikuwa wanakusanya matundwa ya mwitu katika jangwa la mkoa huo wakati walipovamiwa na magaidi wanaoaminika kuwa wanachama wa ISIS na kufyatuliwa risasi.

Mmoja wa manusura watano wa shambulio hilo ameiambia SANA kuwa, magaidi hao waliteketeza kwa moto magari yao. Februari 12, magaidi wa Daesh waliwaua raia wengine 11 na kuteka nyara 75 huko mashariki mwa Syria.

Haya yanajiri siku chache baada ya makumi ya magaidi wa Daesh waliokuwa wamefungwa jela katika gereza moja nchini Syria kutoroka baada ya kufanya uasi kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo na Uturuki.

Gereza hilo la jeshi la polisi linalopatikana katika mji wa Rajo karibu na mpaka wa Uturuki lina wafungwa wasiopungua 2,000; huku 1,300 miongoni mwao wakishukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. 

Hadi sasa karibu watu elfu 45 wameripotiwa kuaga dunia katika tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta lililotokea katika mpaka wa Syria na Uturuki.

 

3482514

captcha