Hizbullah imelitaja tukio hilo kuwa ni uhalifu wa kikatili uliolenga kuvuruga mshikamano wa kitaifa wa Syria na kuchochea machafuko na ukosefu wa usalama nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Hizbullah ilisema kuwa mauaji hayo ya kulengwa yalitekelezwa na watu wahalifu na wasaliti waliolenga kuanzisha migogoro ya kimadhehebu na kidini miongoni mwa jamii mbalimbali za Syria.
Taarifa hiyo ilibainisha kwamba uhalifu huo ulialenga moja kwa moja mwanazuoni aliyejitolea maishani katika kuhudumia Uislamu na taifa la Syria. Sheikh Shahoud alijitolea kulea vijana kielimu na kiimani, alikuwa mlinganizi wa haki, na mtetezi wa wanyonge kwa dhati.
Hizbullah imesisitiza kuwa “Uhalifu huu unapaswa kulaaniwa vikali na taasisi zote za kielimu, kiroho, na kidini.” Harakati hiyo imetoa wito kwa mamlaka husika kuwasaka wahusika na kuwawajibisha kwa uhalifu huo wa kuchukiza.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa yeyote atakayethibitika kuhusika au kushirikiana katika tukio hilo la kigaidi lazima afikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Hizbullah imeongeza kwa kusema: “Tuna uhakika kuwa wananchi wa Syria watakataa kabisa itikadi hii kali ya kigaidi inayotishia mshikamano wa kijamii, kuvuruga uthabiti wa taifa, na kushambulia kila sauti ya wastani na fikra yenye mwanga.”
Usalama nchini Syria umeendelea kuwa tete, hasa baada ya kuingia madarakani kundi la Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), tawi la kundi la kigaidi la al-Qaeda. Matukio ya vurugu za kimadhehebu, ikiwemo mauaji ya mamia ya Waalawi mnamo Machi, yameongeza hofu miongoni mwa jamii za wachache kuhusu uhalisia wa usalama katika taifa hilo lililokumbwa na mizozo.
3493815