IQNA

Ahadi ya Kweli

Onyo la Iran kwa Marekani: Msithubutu kuchukua hatua za kijeshi

16:41 - April 15, 2024
Habari ID: 3478686
IQNA-Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameionya Marekani kuhusu kuanzisha hatua za kijeshi dhidi ya Iran baada ya operesheni yake ya kisheria ya hivi karibuni ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, mshirika mkuu wa kieneo wa Washington.

Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili kwamba Iran haina nia ya kuingia katika mzozo na Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Pamoja na hayo ameonya kuwa: "Ikiwa Marekani itaanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, raia wake au usalama na maslahi yake, Iran itatumia haki yake ya kimsingi kujibu chokochoko."

Tarehe 1 Aprili, utawala wa Israel ulifanya shambulizi la kigaidi dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Shambulio hilo la Israel lilisababisha kuuawa shahidi Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi, kamanda mwandamizi  wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Quds (IRGC), naibu wake, Jenerali Mohammad Hadi Haji Rahimi na maafisa watano walioandamana nao.

Kufuatia hujuma hiyo ya kigaidi, IRGC ilitekeelza operesheni ya kulipiza kisasi kwa kuilenga Israel usiku wa kuamkia Jumapili kwa kutumia ndege na makombora na msururu wa ndege zisizo na rubani. Shambulio hilo la kulipiza kisasi, lililopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli, limesababisha uharibifu katika kambi za kijeshi za Israel katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu, lakini kiwango chake bado hakijabainishwa.

Kufuatia hatua hiyo ya kulipiza kisasi, Iran imetume ujumbe na kusema kwamba imekamilisha ililokusudia huku ikiionya Marekani dhidi ya kujaribu kujihusisha katika mzozo huo.

Kwingineko katika matamshi yake, balozi huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa amezikosoa vikali Marekani na Uingereza na kusema nchi hizo mbili zinawajibika kikamilifu kwa uchokozi na ukiukaji sheria wa Israel kwa miongo kadhaa.

Mjumbe huyo alikuwa akiashiria vita vya sasa vya utawala huo wa Kizayuni  vilivyoanza Oktoba 7 dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambapo hadi sasa jeshi katili la Israel limeua Wapalestina zaidi ya 33,700, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Wakati huo huo, Iravani ametahadharisha kwamba "kutokuwepo uwajibikaji na kutochukua hatua Baraza la Usalama mbele ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel na uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Palestina kumeupa ujasiri utawala huo kuendeleza ukiukaji wake bila kudhibitiwa."

3487942

captcha