IQNA

Mashindano ya fainali ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Iran yaanza Mashhad

17:38 - January 27, 2025
Habari ID: 3480107
IQNA – Hafla ilifanyika Jumapili jioni mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran, kuzindua hatua ya fainali ya Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu nchini humo.

Ukumbi wa Quds wa Haram Tukufu wa Imam Reza (AS) uliandaa hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa na maafisa waandamizi wa kisiasa, Qur’ani na kidini, pamoja na washiriki wa mashindano na wajumbe wa paneli za majaji.

Hafla ilianza kwa kisomo cha aya za Qur’ani Tukufu kilichofanywa na qari wa Iran, Hadi Esfidani, mshindi wa kipengele cha usomaji katika toleo la awali la mashindano hayo.

Akihutubia hafla hiyo, Mkuu wa Shirika la Mambo ya Wakfu na Misaada ya Kijamii, Hojat-ol-Islam Seyed Mehdi Khamouhi, aliwakaribisha wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Alisema, "Tunamshukuru Mungu kwamba mkusanyiko huu unafanyika karibu na (Haram Tukufu ya) Imam Reza (AS) katika mji mtukufu wa Mashhad."

Alitaja kaulimbiu ya mashindano ya mwaka huu, ambayo ni “Qur’ani; Mwongozo wa Pekee wa Ukamilifu”, na kusema kuwa kaulimbiu hii inaangazia nafasi ya Qur’ani kama kitabu kinachoongoza wanadamu kufikia ukamilifu.

Hojat-ol-Islam Khamouhi pia alitoa ripoti juu ya maandalizi ya mashindano hayo, akisema kuwa wasomaji wa Qur’ani na wahifadhi kutoka nchi 144 walishiriki katika hatua za awali, na kati yao, wawakilishi wa nchi 27 wamefuzu kwa fainali.

Jumla ya washindani 59 watachuana ili kushinda zawadi kuu katika hatua ya fainali, alibainisha.

Afisa huyo pia aliwashukuru gavana wa Mkoa wa Razavi Khorasan, msimamizi wa Haram Tukufu ya Imam Reza (AS), na vyombo vya habari kwa ushirikiano wao na mchango wao.

Mashindano hayo yatahitimishwa Ijumaa katika hafla ya kufunga ambapo washindi wa juu watatangazwa na kupewa zawadi.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huandaliwa kila mwaka na Shirika la Mambo ya Wakfu na Misaada ya Kijamii la nchi hiyo.

Mashindano hayo yanakusudia kukuza utamaduni na maadili ya Qur’ani miongoni mwa Waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani.

 

3491621

 

 

 

captcha