IQNA

Wanafunzi Warejea Chuo Kikuu cha Kiislamu Gaza Kilichoharibiwa Baada ya Miaka Miwili

21:00 - December 21, 2025
Habari ID: 3481692
IQNA-Wakipita njia zilizozungukwa na majengo yaliyoharibiwa na vifusi, wanafunzi Wapalestina wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza wiki hii wamerudi darasani kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili.

Kurudi huku ni hatua muhimu ya kufufua maisha ya kielimu, ingawa chuo chenyewe kimebeba alama nzito za vita vya kikatili vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza.

Chuo hiki kilichoko Mji wa Gaza, kilifunguliwa tena baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya Oktoba, na sasa kinahifadhi takriban familia 500 zilizopoteza makazi, ndani ya majengo yaliyogeuka magofu kwa mashambulizi yasiyokoma ya utawala dhalimu wa Israel.

Mahema yameenea katika uwanja ambapo zamani kulikuwa na kumbi za mihadhara, yakionyesha wazi hali mbili za Gaza: ukosefu wa makazi na kuporomoka kwa elimu.

Atta Siam, mmoja wa waliopata hifadhi chuoni, alisema: “Tulikuja hapa baada ya kufukuzwa Jabalia kwa kuwa hatukuwa na pa kwenda. Lakini mahali hapa ni maalumu kwa elimu, siyo kwa hifadhi – ni sehemu ya watoto wetu kusoma.”

Kuanza tena kwa sehemu ya masomo kumezindua matumaini kwa maelfu ya wanafunzi, licha ya mazingira yasiyo fanana na chuo kikuu cha kawaida.

UNESCO inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 95 ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika Ukanda wa Gaza vimeharibiwa vibaya au kuangamizwa tangu Israel ianzishe vita vita vya maangamizi ya kimbari Oktoba 2023.

Youmna Albaba, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa udaktari, alisema: “Nilitamani kusoma katika chuo kilicho na vifaa kamili. Lakini sijapata nilichotarajia hapa. Hata hivyo nina matumaini kwa kuwa tunajenga kila kitu upya.”

Mashirika ya haki za binadamu na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza hali hii kama “scholasticide” – yaani kuangamizwa kwa mfumo mzima wa elimu. Zaidi ya wanafunzi 750,000 wa Kipalestina wamekosa masomo kwa miaka miwili mfululizo, kwa mujibu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Al Mezan kilichoko Gaza.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha hali ya kutisha: shule na vyuo vikuu 494 vimeharibiwa kwa sehemu au kuangamizwa kabisa, huku 137 vikiwa vimegeuka kifusi. Miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanafunzi 12,800, walimu na wafanyakazi wa elimu 760, pamoja na wasomi na watafiti 150.

Chuo Kikuu cha Isra, ambacho kilikuwa chuo cha mwisho kinachofanya kazi Gaza, kilibomolewa na majeshi ya Israel Januari 2024.

Katika Chuo Kikuu cha Kiislamu, maprofesa wanabuni mbinu za dharura katikati ya ukosefu wa umeme, vifaa na mazingira duni ya kusomea. Dkt. Adel Awadallah alieleza jinsi walivyofunika kuta wazi kwa plastiki ili kuwapokea wanafunzi wengi iwezekanavyo. “Tumekopa injini za umeme kuendesha vifaa vya chuo,” alisema.

Kwa vyumba vinne pekee vinavyofanya kazi, maelfu ya wanafunzi wanategemea mipango hii ya dharura kuendeleza masomo yao.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walionya Aprili 2024 kuwa kiwango cha uharibifu kinaweza kuwa jaribio la makusudi la Israel la  kuvunja misingi ya jamii ya Kipalestina. “Shule zikiharibiwa, ndoto na matumaini pia huangamia,” walieleza, wakitaja mashambulizi haya kama ukatili wa kimfumo dhidi ya miundombinu ya elimu.

Changamoto haziko tu katika uharibifu wa majengo. Familia zikihangaika kupata chakula, maji na dawa, zinajikuta haziwezi kusaidia elimu ya watoto wao.

Mipango ya masomo kwa njia ya mtandao ya Wizara ya Elimu na UNRWA imevurugwa na kukatika kwa umeme, intaneti na uhamisho wa watu.

Hata hivyo wanafunzi wanavumilia. Licha ya maumivu ya zaidi ya miaka miwili ya mabomu na kupoteza wapendwa, wametaja kurudi shuleni kama kipaumbele cha juu – nafasi ya kurejesha hali ya kawaida na mustakabali wao.

Kama alivyosema Youmna Albaba: “Licha ya yote haya, nina furaha kwa kuwa nahudhuria mihadhara ana kwa ana. Tunajenga kila kitu upya.”

3495807

Habari zinazohusiana
captcha