IQNA

“Dawlat al-Tilawa” Yasifu Huduma za Qur’an za Marehemu Qari Sheikh Mustafa Ismail

20:56 - December 21, 2025
Habari ID: 3481691
IQNA--Katika kipindi cha wiki hii cha televisheni ya Qur’an nchini Misri, Dawlat al-Tilawa, sehemu maalum ilitengwa kumuenzi marehemu Qari mashuhuri Sheikh Mustafa Ismail kwa huduma zake za Qur’ani.

Kipindi kipya kilirushwa kupitia vituo vya satelaiti vya Misri Ijumaa jioni (Disemba 19). Sheikh Mustafa Ismail alielezewa kuwa miongoni mwa maqari mashuhuri wa Misri wa zama za kisasa, aliyewavutia Waislamu duniani kwa sauti yake tamu na yenye ustadi wa hali ya juu.

Ilisisitizwa kuwa sauti yake ya Qur’ani ilikuwa ni neema kutoka mbinguni, inayogusa nyoyo kwa uzuri na hisia za kiroho. Watangazaji walirejelea wasifu na urithi wake wa Qur’an, wakisema alikuwa mbunifu katika tilawa na mwenye mtindo wa kipekee uliounganisha hifdh ya kina ya aya na ufahamu sahihi wa maana za Qur’ani.

Katika sehemu nyingine ya kipindi, mtangazaji Aya Abdul Rahman aliashiria juhudi za Kamati ya Mapitio ya Qur’an ya Al-Azhar, akieleza kuwa kituo hiki ndicho kinacholinda Qur’ani Tukufu nchini Misri. Alimsifu Sheikh Hassan Abdel Nabi, Qari mashuhuri na mjumbe wa majaji wa mashindano ya Qur’an, ambaye amejitolea maisha yake kulinda Neno la Allah na ni mwanachama wa kamati hiyo.

Kamati hii hutekeleza jukumu la kulinda maandiko ya Qur’an kwa njia ya kielimu, kiteknolojia na kwa umakini mkubwa, ikifuatilia na kukagua shughuli za taasisi yoyote inayotaka kuchapisha Qur’an Tukufu, na kutoa leseni kwa mashirika hayo.

Sehemu nyingine ya kipindi ilihusisha tilawa ya kijana Qari Mohamed al-Qalaji, aliyesoma kwa ustadi mkubwa wa kanuni za Tajwid. Tilawa yake ilipokelewa kwa shangwe na kusifiwa na kamati ya majaji.

Mtaalamu wa sauti na Qur’an, Taha Abdel Wahab, alimsifu al-Qalaji akisema kila mara husisimka na utendaji wake, kwani tilawa yake huwasilishwa kwa ustadi, kujiamini na ubora wa kipekee. Alimtakia mafanikio ya kudumu katika kuhudumia Qur’an Tukufu.

Sheikh Hassan Abdel Nabi, naibu wa Kamati ya Mapitio ya Qur’an ya Al-Azhar na mjumbe wa majaji, pia alimsifu al-Qalaji kwa kuzingatia kanuni za Tajwid, ingawa wakati mwingine alilazimisha sauti yake. Taha al-Numani, mjumbe mwingine wa majaji, alisema: “Mwenyezi Mungu akulinde na aongezee wengine kama wewe, na akufanye jua linaloangaza anga ya tilawa ya Misri.”

Mhubiri wa Kiislamu Mustafa Hassani alisisitiza umuhimu wa subira na uvumilivu katika kukuza vipaji, akisema: “Fanya hili kanuni ya maisha yako: chochote unachofanya, endelea kwa juhudi ile ile, na kwa idhini ya Allah utaona matunda ya juhudi zako siku baada ya siku.”

Kipindi cha Dawlat al-Tilawa kinazalishwa kwa ushirikiano na Wizara ya Awqaf na Kampuni ya Huduma za Vyombo vya Habari nchini Misri, kwa lengo la kubaini vipaji na makari bora kutoka mikoa mbalimbali ya nchi.

Kipindi hurushwa kupitia vituo vya satelaiti vya Al-Hayat, CBC, Al-Nas, Misr al-Qur’an al-Karim, na jukwaa la “watch it”, saa 3 usiku kila Ijumaa na Jumamosi.

Mashindano haya yanatoa jumla ya zawadi ya paundi milioni 3.5 za Misri. Washindi wa kwanza katika vipengele vya tilawa na naghma watapokea kila mmoja paundi milioni moja, na Qur’an nzima itarekodiwa kwa sauti zao na kurushwa kupitia kituo cha “Misr Qur’an Karim”. Pia watapewa heshima ya kuongoza swala za Taraweeh katika Msikiti wa Hussein katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ujao.

Kamati ya majaji inajumuisha wanazuoni na viongozi mashuhuri wa Kiislamu: Hassan Abdel-Nabi, Taha Abdel-Wahab, Mostafa Hosny, na Taha al-Numani. Wageni maalum ni pamoja na Osama al-Azhari, Nazir Mohamed Ayyad, Ali Gomaa, Ahmed Na’ina, Abdel-Fattah al-Tarouti, Jaber al-Baghdadi, mwanazuoni wa Kiingereza Muhammad Ayoub Asif, na Qari mashuhuri wa Morocco Omar al-Qazabri.

3495804

captcha