Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, meya wa mji wa Boda amesema kuwa, Wakristo wenye misimamo mikali wa kundi la Anti Balaka wametishia kuwa, watawaua Waislamu iwapo hawatoondoka kwenye mji huo.
Mji wa Boda uko kilomita 160 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wa Bangui na katika mji huo kuna Waislamu karibu 4,000. Wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka pia wameipa serikali pamoja na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika muda wa masaa 48 eti wawe wamesitisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo, la sivyo jamii ya kimataifa ndio itajibu hali mpya itakayotokea nchini humo.
Hayo yanajiri huku Umoja wa Ulaya ukisema kuwa upo tayari kupeleka askari katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kusaidia kutuliza hali ya mambo ya nchi hiyo. EU inapanga kutuma askari 800 hadi 1,000 ili kuungana na askari 6,000 wa Kiafrika na 2,000 wa Ufaransa ambao tayari wako Jamhuri ya Afrika ya Kati.