IQNA

Waislamu waendelea kuukimbia mji wa Bangui

17:51 - April 22, 2014
Habari ID: 1398695
Hali ya usalama katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, inazidi kuwa mbaya huku vitendo vya mauaji dhidi ya Waislamu vikiendelea kuripotiwa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA,taarifa zaidi kutoka Bangui zinasema kuwa, Waislamu wameendelea kuukimbia mji huo kutokana na kuendelea kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka. Waislamu hao wanaukimbia mji huo na kukimbilia katika nchi jirani za Chad na Cameroon ili kuokoa maisha yao.

Ripoti zaidi kutoka nchini humo zinasema kuwa, makundi kwa makundi ya Waislamu wanaonekana kila siku wakiimbia nchi hiyo na kwenda kuomba hifadhi katika nchi jirani.

Wakati huo huo viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wametangaza kuwa, Umoja wa Mataifa umewahamisha Waislamu zaidi ya 100 kutoka Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo na kuwapeleka kwenye maeneo mengine yenye usalama.

Maafisa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kuokoa maisha ya Waislamu, ambao maisha yao yako hatarini kutokana na kuandamwa na mashambulio ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka.

1398631

captcha