Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa muungano huo imeeleza kuwa, kundi la Daesh linatekeleza dhuluma kubwa kwa kuua na kumwaga damu za watu wasio na hatia kwa jina la Uislamu na kulitaka kundi hilo kumuogopa Mwenyezi Mungu na kuacha kikamilifu kutenda jinai kwa jina la Uislamu. Katibu Mkuu wa Muungano wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani amesema kuwa, hatua ya Daesh ya kusababisha maelfu ya wananchi wa Syria na Iraq kuwa wakimbizi inakinzana vikali na misingi ya dini ya Kiislamu, kwani kumfukuza mtu kwenye makazi yake ni miongoni mwa dhambi kubwa. Wakati huohuo, zaidi ya wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu mia moja katika ulimwengu wa Kiislamu, wamemuandikia barua Ibrahim A'wad al Badri mwenye lakabu ya 'Abubakar al Baghdadi' kiongozi wa Daesh na kumueleza kwamba, vitendo vya Daesh vinakinzana na sheria za dini ya Kiislamu. Jopo hilo la mwanazuoni na wanafikra wa umma wa Kiislamu limelaani vikali kutumiwa jina la jihad katika operesheni za kijeshi za Daesh na kusema kwamba vita vya jihad hutumika kwa ajili ya kujilinda na hutangazwa katika hali maalumu, ambapo kundi la Daesh halina sifa hizo.../mh