IQNA

Vita dhidi ya ugaidi

Nchi za Kiislamu zaendelea kulaani hujuma ya kigaidi dhidi ya Maulidi nchini Pakistan

19:19 - September 30, 2023
Habari ID: 3477670
Nchi za Kiislamu zimelaani vikali mashambulizi mawili ya kigaidi ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi nchini Pakistan.

Siku ya Ijumaa, takriban watu 52 waliuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi dhidi mkusanyiko wa kidini wa Maulidi wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) katika mkoa wa Balochistan nchini Pakistan.

Baadaye mchana, mlipuko ulikumba msikiti mmoja katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa unaopakana na Afghanistan, na kuua takriban watu watano.

Katika ujumbe wake wa pole kwa Rais Arif Alvi wa Pakistan, Rais wa Iran Sayyid Ebrahim Raisi amesema 'Matendo pofu kwa mara nyingine yameonyesha namna magaidi ambao hawana ufahamu wowote kuhusu mafundisho ya rehema ya Uislamu, hawana malengo yoyote isipokuwa kuibua mifarakano miongoni mwa Waislamu."

Aidha Sayyid Raisi ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Pakistani hususan kwa wahanga hujuma hizo, na kuwaombea ahueni ya haraka majeruhi wa mashambulizi hayo ya kikatili ya jana. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kushirikiana na Pakistan katika vita dhidi ya aina zozote za ugaidi na misimamo mikali ya kufurutu ada.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamiii ya kimataiifa hasa mataifa ya Waislamu kutoa radiamali zao madhubuti dhidi ya vitendo hivyo vya kikatili, ili visijikariri.

Uturuki pia ililaani mashambulizi hayo, ikieleza kusikitishwa na kupoteza maisha.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake, "Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kwamba, zaidi ya watu 50 walipoteza maisha, na zaidi ya watu 100 walijeruhiwa katika shambulio dhidi ya jamii iliyokusanyika kwa ajili ya sherehe za Milad un-Nabi kwenye msikiti mnamo Septemba 29, 2023, katika mkoa wa Mastung katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan,"

"Tunalaani shambulizi hili baya lililolenga mahali pa ibada katika siku hii takatifu na tunawatakia rehema za Mwenyezi Mungu waliopoteza maisha, tunatuma salamu za rambirambi kwa familia za wahasiriwa na tunawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa katika shambulio hilo," ilisema taarifa, na kuongeza kuwa Uturuki inaungana katika huzuni ya Pakistan juu ya shambulio hilo.

Aidha taarifa hiyo imesema Uturuki itaendelea kuunga mkono Pakistan kwa dhamira katika mapambano yake dhidi ya ugaidi, ilisisitiza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia pia imelaani vikali miripuko hiyo ya kigaidi nchini Pakistan.

Imetuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia wa wahasiriwa, ikitaja hujuma hiyo ya kigaidi kuwa ya kiwoga.

3485363

Kishikizo: pakistan ugaidi kigaidi
captcha