Shirika la Kimataifa la Habari la Quran IKNA, likinukulu gazeti la Al Watan la Kuwait limeandika kuwa, mfumo wa benki wa Kiislamu sasa unakubalika na waliowengi duniani na kwamba hivi sasa wataalamu wa kiuchumi Waislamu ndio wanaoweza kuunusuru ulimwengu kutoka mgogoro wa sasa wa kifedha kwa kufuata mfumo wa kifedha za Kiislamu.
Gazeti la Washington Post limemnukulu Ahmad Baqir Waziri wa Biashara wa Kuwait akisema kuwa 'mgogoro wa kifedha uliopo duniani umepelekea baadhi ya nchi kutumia misingi na mfumo wa benki za Kiislamu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ahmad Baqir amesema chimbuko la mfumo wa kifedha wa Kiislamu ni Quran Tukufu. Ameongeza kusema kuwa, Uislamu umeharamisha riba na unasisitiza kuwa utajiri lazima upatikane kupitia uwekezaji na mipango ya uzalishaji.
Pamoja na hayo, Waziri wa biashara wa Kuwati amekumbusha kuwa mashirika ya Kifedha ya Kiislamu hayawekezi katika uzalishaji usiojuzu kama vile wa nyama ya ngurue, sigara, suhula za kamari, pombe na utengenezaji silaha.
Mwishoni mwa ripoti yake , gazeti la Washington Post limeashiria safari aliyoifanya huko Saudia Arabia wiki iliyopita Stuart Levey Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani na kuandika kuwa; 'katika safari hiyo Levey alisema wataalamu wa wizara ya fedha ya Marekani wanachunguza uwezekano wa kutekeleza mfumo wa kifehda na kibenki wa Kiislamu huko Marekani'.
313875