IQNA

Mradi wa “Kutoka Arubaini hadi Arubaini” wazinduliwa katika Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS)

18:17 - May 23, 2026
Habari ID: 3482273
IQNA – Uongozi (Mfawidhi) wa Haram tukufu ya Imam Hussein (AS) umetangaza utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa muundo wa zege wa uwanja wa Imam Hassan al-Mujtaba (AS). Mradi huu utatekelezwa kwa jina la “Kutoka Arubaini hadi Arubaini” na unatarajiwa kuzinduliwa mwanzoni mwa mwezi wa Rabi’ al-Awwal 1448 Hijria (Agosti 14, 2026).

Hossein Reza Mahdi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo katika uongozi huo, amesema kuwa shughuli za ujenzi katika viwanja vya Hazrat Zaynab (SA) na Imam Hassan al-Mujtaba (AS) zinaendelea vizuri na zimefikia hatua nzuri ya maendeleo.

Amesema kuwa, kwa ajili ya sehemu iliyobaki ya mradi huo, ombi liliwasilishwa kwa Msimamizi wa Haram hiyo, Sheikh Abdul Mahdi al-Karbalai, la kujenga kikamilifu uwanja wa Imam Hassan al-Mujtaba (AS) wenye eneo la zaidi ya mita za mraba 90,000 ndani ya mwaka mmoja, na idhini yake imeshapatikana.

Bwana Mahdi ameongeza kuwa, baada ya kumalizika kwa maadhimisho ya Eid al-Ghadir yajayo, mkutano utafanyika ili kupitia kwa kina maelezo ya mradi huo na kuandaa mpango kazi wa “Kutoka Arubaini hadi Arubaini.” Mkutano huo utabainisha huduma na vifaa vitakavyotolewa kwa ajili ya mazuwaru (wafanyaziyara), huku lengo kuu likiwa ni kukamilisha kwa ukamilifu uwanja wa Imam Hassan al-Mujtaba (AS).

Katika ziara ya hivi karibuni ya Sheikh al-Karbalai katika eneo la mradi huo, alisisitiza umuhimu wa ubora wa kazi na kupongeza juhudi kubwa na za kutukuka za wafanyakazi wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huu.

4353662

captcha