IQNA

Guardiola: Kocha wa soka anayetetea Palestina

18:30 - May 23, 2026
Habari ID: 3482274
IQNA – Kuanzia Gaza hadi Catalonia, Pep Guardiola amedhihirisha kuwa anaamini mambo makubwa zaidi ya soka. Kocha huyo wa Manchester City amejipatia sifa duniani kama mmoja wa watu mashuhuri wanaosimama kidete kutetea haki za watu wa Palestina.

Ikiwa Bill Shankly, kocha mashuhuri wa zamani wa Liverpool, aliamini kuwa soka ni “kitu muhimu zaidi” kuliko maisha au kifo, kwa Guardiola, kuna mambo mengi nje ya uwanja wa soka ambayo yana uzito mkubwa vilevile.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 55, anatarajiwa kuondoka kwenye benchi la ufundi la Manchester City siku ya Jumapili, baada ya kushinda mataji 20 katika kipindi cha miaka 10.

Katika kipindi chote hicho, Guardiola amekuwa akitumia nafasi yake kusemea mambo mbalimbali yanayogusa jamii; kuanzia masaibu ya watoto wa Palestina, harakati za kujitawala eneo Catalonia, hadi tatizo la watu wasio na makazi nchini Uingereza. Hajawahi kusita kutumia jukwaa lake la soka kama sauti ya “kujenga jamii bora.”

Hatua yake ya hivi karibuni ya kujitolea kutetea hali ngumu inayowakabili watoto wa Palestina huko Gaza, katikati ya vita vya mauaji ya kimbari vinavyofanywa na utawala wa Israel, imezidi kuonyesha ujasiri wake.

Vita hivyo vilivyoanza mwezi Oktoba 2023, vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 72,568 huko Gaza, wengi wao wakiwa watoto. Mamia ya maelfu ya watu wamebaki bila makazi na wanaishi kwenye mahema, hali ikiwa mbaya sana licha ya kusitishwa kwa mapigano mwezi Oktoba.

Uharibifu huu umewaathiri zaidi watoto, jambo ambalo Guardiola aliliona kuwa muhimu kiasi cha kukosa mkutano wa wanahabari kabla ya mechi ili kuhudhuria tukio la hisani la “Act x Palestine” huko Barcelona mnamo mwezi Januari mwaka huu. Akiwa amejifunga keffiyeh (kilemba cha utambulisho wa Palestina) shingoni mwake, alitoa ujumbe mzito:

“Ninapowaona watoto hawa kupitia picha za mitandao ya kijamii na televisheni wakijiuliza ‘mama yangu yuko wapi?’ katikati ya vifusi, nawaona wakiwa wameachwa peke yao, wametelekezwa.”

Ingawa amepata pongezi nyingi, msimamo wake pia umekutana na upinzani, hasa kutoka kwa wawakilishi wa jamii ya Kiyahudi mjini Manchester, ambao walimwandikia barua mwenyekiti wa Manchester City wakidai kauli zake zinahatarisha usalama wa Wayahudi jijini humo.

Hata hivyo, Guardiola hajawahi kuyumba, kama ilivyokuwa mwaka 2018 alipopigwa faini ya Pauni 20,000 kwa kuvaa utepe wa manjano kuunga mkono wanasiasa waliofungwa gerezani katika jimbo la Catalonia nchini Hispania.

Sio tu masaibu ya watoto wa Palestina yaliyomfanya ajitokeze; mnamo mwezi Februari, alikemea vikali ukatili unaoendelea Mashariki ya Kati, Ukraine, Sudan, na hata mauaji yaliyofanywa na maajenti wa idara ya uhamiaji ya ICE nchini Marekani.

“Unapoua maelfu ya watu ili kutetea itikadi yako, samahani, mimi nitasimama kidete,” alisema Guardiola. “Daima, nitasimama upande wa haki.”

captcha