IQNA

Ibada ya Hija : Nembo ya Siasa katika Uislamu

18:36 - May 23, 2026
Habari ID: 3482275
IQNA – Mkuu wa ujumbe wa Hija wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametaja ibada ya Hija kama nembo kuu ya siasa katika Uislamu

Akizungumza katika mkutano wa watumishi wa Hija wa Iran mjini Makka siku ya Ijumaa, Hujjatul-Islam Seyed Abdol Fattah Navab, mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Hija na Ziara, amesema kuwa baadhi ya watu wanajaribu kutenganisha ibada ya Hija na siasa, jambo ambalo linakinzana na mafundisho ya kweli ya Uislamu.

“Kwa mujibu wa Imam aliyeuawa shahidi (Ayatullah Seyed Ali Khamenei), asili ya mkusanyiko wa mahujaji katika wakati mmoja na mahali pamoja, wakiwa na programu moja na wajibu mmoja, ndiyo alama kuu ya siasa katika ibada za Kiislamu. Siasa si kitu kingine zaidi ya kubainisha ‘mambo ya kufanya na yale ya kuyaepuka’ kwa ajili ya ustawi na saada ya jamii,” alisisitiza Hujjatul-Islam Navab.

Akisisitiza kanuni ya Qur’ani ya kuwa “wenye huruma wao kwa wao,” amenukuu kauli ya Kiongozi wa Mapinduzi akisema kuwa Hija ya kweli ni ile inayobeba sifa za “Hija ya Nabii Ibrahimu”.

Ameongeza kuwa: “Umoja, ushirikiano, mshikamano, kutilia maanani masuala ya Waislamu, hasa wenzetu wa Palestina wanaodhulumiwa, pamoja na kujitenga na maadui wa Uislamu, ni mambo yaliyojificha ndani ya Hija ya Kiibrahimu.”

Hujjatul-Islam Navab amebainisha kuwa kwa takriban miezi mitatu sasa, wananchi wa Iran wamekuwa wakijitokeza kwenye viwanja vya miji yao, wakipaza sauti dhidi ya maadui na kusimama kidete. Ametaja kuwa adui ameona muqawama (mapambano) na uthabiti huu.

“Sasa, kama Waislamu wote duniani wangejitokeza kwa umoja kwenye viwanja hivi, maadui bila shaka wangewatazama Waislamu kwa jicho tofauti. Hii ndiyo Hija ya Kiibrahimu ambayo Imam Shahidi alizungumzia,” alihitimisha.

3497564

Kishikizo: hija ibada
captcha