IQNA

Fitina ya kimadhehebu njama ya Marekani kwa ajili ya kuwadhoofisha Waislamu

9:20 - November 09, 2008
Habari ID: 1705993
Kueneza hitilafu na fitina miongoni mwa Washia na Wasunni ni sehemu moja ya njama za kiuadui za Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuonyesha kwamba Waislamu ni dhaifu na kwamba hawana uwezo wa kusimama mbele ya madola ya kibeberu ulimwenguni.
Hayo yalisemwa jana na Sheikh Naeem Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchini Lebanon Hizbullah, alipokutana na kuzungumza na Abubakr Fofana, mkuu wa Baraza Kuu la Maimamu wa Misikiti nchini Ivory Coast. Amesema kuwa baada ya kuwaona Waislamu wanafanya juhudi za kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao na kupigania kujitawala kwa nchi zao, madola ya kibeberu na yenye kiburi duniani yamekuwa yakitumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya kisiasa ya Waislamu ili kuvuruga kabisa mipango yao. Sheikh Qassim amesema kuwa baada ya maadui hao kuona kwamba njia za kijeshi haziwasaidii wala kuwaletea natija ya kuridhisha wameanza kutumia njia za kuzusha fitina na hitilafu za kimadhehebu miongoni mwa Waislamu ili kufikia malengo yao haramu katika nchi za Kiislamu. Huku akiashiria kwamba Waislamu wana mtazamo mzuri sana wa kisiasa na kidini, Sheikh Naeem Qassim amesisitiza kwamba makundi mbalimbali ya kidini na kikabila ya Lebanon yamethibitisha kwamba hayawezi kuathiriwa na hitilafu za kidini na kwamba mapambano yao dhidi ya uchokozi wa utawala haramu wa Israel ni uthibitisho wa wazi wa mshikamano na umoja wa wananchi hao. Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Sheikh Ali Damush, Mkuu wa Uhusiano wa Nje wa Hizbullah na Sheikh Jibril Siseh, Mkuu wa Uhusiano wa Nje wa Baraza Kuu la Maimamu wa Ivory Coast, kilichunguza matatizo yanayowakabili Waislamu katika hali ya hivi sasa na masuala yanayohusiana na umuhimu wa kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbili muhimu za Kiislamu za Shia na Sunni. 317101
captcha