IQNA

Kuanzishwa kitengo cha "Fiqhi Linganishi" katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh nchini India

14:41 - November 17, 2008
Habari ID: 1709302
Kitengo cha mafunzo ya ‘Fiqhi Linganishi’ kinatazamiwa kuanzishwa hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh nchini India kwa ushirikiano wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran mjini New Delhi Karim Najafi amesema kuwa pendekezo la kuanzishwa kitengo cha Fiqhi Linganishi katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh limetolewa na Mkuu wa Kitivo cha Teolojia wa chuo hicho Saud Alim Qasimi na kwamba kitengo hicho kitaanzishwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlulbaiti, Chuo Kikuu cha Madhehebu za Kiislamu na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu.
Karim Najafi amesema, lengo la kuanzisha kitengo hicho ni kuwaelimisha wanafunzi fiqhi ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu na kuwawezesha kufahamu fiqhi ya Ahlubaiti wa Mtume Muhammad SAW. Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran nchini India amesema, kitengo hicho kitafanya utafiti kuhusu fiqhi linganishi na kwamba wanafunzi wataweza kufanya mlinganisho wa fiqhi za madhehebu yote ya kifiqhi ya Kiislamu kama Hanaji, Shafi, Hanbali, Maliki na Jaafari. Amesema kuwa pande hizo mbili vilevile zimefikia makubaliano ya kubadilishana wahadhiri kati ya Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh na vituo vya kielimu vya Iran, ushirikiano katika nyanja za maarifa ya Kiislamu na kuchapisha vitabu vya taaluma mbalimbali, kuitisha mikutano ya kimataifa ya kidini na kutayarisha vikao vya mazungumzo kati ya dini mbalimbali. 321243
captcha