IQNA

Rais Pezeshkian Akihutubia UNGA: Hujuma ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ilikuwa usaliti kwa diplomasia

9:42 - September 25, 2025
Habari ID: 3481282
IQNA-Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya anga ya “kikatili” yaliyofanywa na Marekani na Israel mwezi Juni katika ardhi ya Iran na kusema yalikuwa usaliti kwa diplomasia.

Ametoa kauli hiyo Jumatano wakati wa hotuba yake kwenye kikao cha 80 cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Rais wa Iran amesema mashambulizi hayo yalikuwa “pigo kubwa” kwa imani ya kimataifa na amani ya kikanda. Rais Pezeshkian ameongeza kuwa mashambulizi hayo, ambayo yalilenga miji ya Iran, nyumba za raia na miundombinu huku mazungumzo ya kidiplomasia yakiendelea, yalikuwa “usaliti mkubwa wa diplomasia na kudhoofisha juhudi za kuimarisha amani na uthabiti.”

Akiwa ameinua picha za wahanga mbele ya hadhira rais wa Iran amesema: “Mnayoona katika picha hizi za mauaji na uhalifu ni mauaji ya watoto na wanawake. Ni rekodi mbaya ya ukatili uliofanywa na Israel katika nchi yetu dhidi ya watu wetu, wakiwemo wanawake, watoto na vijana, kwa jina la kulinda amani na usalama wa eneo."

Rais Pezeshkian amesisitiza ustahimilivu wa Iran, akisema taifa hili ni “ustaarabu wa dunia ulioendelea bila kukatizwa kwa muda mrefu zaidi” na limehimili dhoruba za kihistoria.

Amesema: “Licha ya vikwazo vya kiuchumi vilivyo vikali zaidi, virefu, na vizito, vita vya kisaikolojia, kampeni za propaganda za vyombo vya habari, na juhudi za daima za kuleta mgawanyiko, baina ya watu wa Iran, tangu risasi ya kwanza ilipopigwa katika ardhi yao, walisimama pamoja nyuma ya vikosi vyao jasiri vya ulinzi, na leo wanaendelea kuheshimu damu ya mashahidi wao."

Rais wa Iran pia amegusia kadhia ya Palestina na kusema kuwa Marekani na Israel wamemwaga damu ya maelfu ya watu wasio na hatia huko.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita dunia imeshuhudia mauaji ya kimbari Gaza; uharibifu wa nyumba na ukiukwaji wa mara kwa mara wa uhuru na mipaka ya Lebanon; kuangamizwa kwa miundombinu ya Syria; mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen; njaa ya kulazimishwa kwa watoto wakiwa mikononi mwa mama zao; hujuma dhidi ya uhuru wa mataifa, ukiukwaji wa mipaka ya kieneo ya nchi, na kulengwa wazi kwa viongozi wa kitaifa.

Rais wa Iran ameonya kuwa ikiwa “ukiukaji hatari” kama huu hautakemewa, utaenea duniani kote.

Rais Pezeshkian amelaani mpango mbovu wa “Israel Kubwa,” akiishutumu Israel kwa kuendeleza uchokozi na ubaguzi wa rangi chini ya kivuli cha “amani kupitia nguvu.”

Amesisitiza tena msimamo wa muda mrefu wa Iran wa kutaka Asia Magharibi isiwe na silaha za maangamizi, huku akikosoa mataifa yenye silaha za nyuklia kwa kukiuka Mkataba wa Kutokuzalisha Silaha za Nyuklia (NPT) huku wakati huo huo yakiishinikiza Iran kwa “tuhuma zisizo na msingi.”

Akigeukia mvutano kuhusu utaratibu wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran unaojulikana kama “snapback” katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, Rais Pezeshkian amelaani nchi tatu za Ulaya kwa kujaribu kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama vya Umoja wa Mataifa vilivyokuwa vimefutwa dhidi ya Tehran, akitaja hatua hiyo kuwa “isiyo halali” na iliyofanywa “kwa amri ya Marekani.”

Amesisitiza kwamba Iran haijawahi kutafuta silaha za nyuklia ambapo ameashiria amri ya kidini au fatwa ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu uharamu wa kumiliki silaha za nyuklia.

Akitoa wito wa mtazamo mpya wa usalama, amewasihi viongozi wa dunia wakumbatie “kuaminiana, kuheshimiana na mshikamano wa kikanda” badala ya matumizi ya nguvu.

Rais wa Iran amehitimisha kwa kutoa mwito wa kurejesha heshima ya taasisi za kimataifa na kuanzisha mfumo wa usalama wa kikanda katika Asia Magharibi.

“Turejeshe na tujenge upya heshima ya taasisi za kimataifa na mifumo ya kisheria, na tuthibitishe dhamira ya kuanzisha mfumo wa usalama na ushirikiano wa kikanda katika Asia Magharibi.”

4306892

captcha