IQNA

Gazeti la Le Monde Diplomatique lakaribisha mazungumzo na wanafikra wa Kiislamu

10:08 - November 19, 2008
Habari ID: 1710058
Gazeti la Le Monde Diplomatique ndilo gazeti pekee la Ufaransa ambalo linajadili na kuchunguza kwa kina matatizo ya Waislamu, fikra zao na kuunga mkono kufanyika mazungumzo na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu nchini humo.
Hayo yamesemwa na Michel Raffole, mwakilishi wa gazeti hilo katika maonyesho ya magazeti na mashirika ya habari mjini Tehran. Amesema kuwa, gazeti hilo limekuwa likikabiliana kwa njia nzuri na Waislamu wa Ufaransa na kuchunguza pamoja na kuakisi matatizo yanayowakabili kwa uadilifu mkubwa. Amesema kuwa, gazeti la Le Monde limekuwa likifanya mazungumzo na mahojiano ya mara kwa mara na wanafikra mashuhuri wa Kiislamu nchini Ufaransa, akiwemo Tariq Ramadhan, ambao wana mtazamo mpana na ujuzi mkubwa kuhusiana na jamii mbili za Magharibi na Mashariki. Amesema, magazeti mengi ya Ufaransa yanakwepa kufanya mahojiano kama hayo na Waislamu na kulichukulia jambo hilo kuwa linaloeneza fikra za Kiislamu nchini humo. Amesema, kinyume na hatua za magazeti hayo, gazeti la Le Monde huchunguza kwa kina matatizo na fikra za jamii ya Kiislamu ya nchi hiyo na kujaribu kuwafahamisha Wamagharibi mitazamo sahihi kuhusiana na mafundisho halisi ya Uislamu. Michele Raffole amesisistiza kwamba, kuna haja kubwa kwa viongozi na wanafikra wa Kifaransa kufanya juhudi za kujua itikadi halisi za jamii ya Waislamu wa nchi hiyo kwa kuzingatia kuwa Ufaransa ndiyo nchi iliyo na idadi kubwa zaidi ya Waislamu kati ya nchi zote za Ulaya, na kwamba Uislamu ndiyo dini ya pili kwa ukubwa nchini humo. Amesema, nukta nyingine inayotoa fursa kwa Wafaransa na jamii zote za Ulaya kutaka kujua itikadi na fikra za Kiislamu ni kuwa, Waislamu ndio wanaounda idadi kubwa zaidi ya wahajiri nchini Ufaransa. Amesema mambo hayo yanawajibisha wanafikra na wasomi wa Ufaransa kufanya vikao mbalimbali vya majadiliano na mazungumzo na wasomi wenzao wa Kiislamu. 322129
captcha