IQNA

Kutumiwa vibaya dini kwa malengo ya kisiasa kunazuia ujumbe wa vyombo vya habari

8:06 - November 22, 2008
Habari ID: 1710786
Serikali na tawala ambazo kidhahiri zinaonekana kuwa za kidini daima zimekuwa zikitumia vibaya hisia za wafuasi wa dini kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
Hii leo pia utumiaji huo mbaya wa dini kwa lengo la kudhamini maslahi ya kisiasa, umeingia katika awamu mpya na hivyo kuzuia kuthibiti kwa malengo ya vyombo vya habari. Akizungumza na mwandishi habari wa Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa pambizoni mwa Tamasha la 15 la Kimataifa la Magazeti na Mashirika ya Habari ambalo lionamalizika leo Jumamosi mjini Tehran, Khudhar Majid, mkuu wa kitengo cha utafiti cha Wizara ya Habari ya Lebanion na mwakilishi wa nchi hiyo katika tamasha lililotajwa, amesema kuwa dini zote za mbinguni na hasa za Uyahudi, Ukristo na Uislamu zimekuwa zikiishi pamoja kwa amani na kwamba watawala na viongozi wenye tamaa ndio wamekuwa wakizitumia vibaya ili kuzusha fitina na migawanyiko miomngoni mwa wafuasi wao kwa shabaha ya kudhamini malengo yao ya kisiasa. Amesema, propaganda za nchi za Magharibi zimeulenga Uislamu ikiwa dini muhimu na inayoenea kwa kasi kubwa zaidi ulimwenguni. Hata hivyo, amesema kuwa hujuma kubwa ya propaganda inayoendeshwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi si ngeni bali ilikuwepo hata katika kipindi cha Mtume Mtukufu (saw) na Maimamu watoharifu (as). Amesema, hujuma hiyo imepata msukumo mkubwa kutoka kwa ubeberu mambo-leo na magenge ya Kizayuni na hivyo kuwa hatari kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vya Magharibi vimepotosha kabisa sura halisi ya Uislamu kwa kudai kwamba ni ugaidi, na kuwa huo ndio mtazamo wa Wamagharibi waliowengi ambao wanaviamini vyombo hivyo. Hii ni katika hali ambayo, dini hii ya Mwenyezi Mungu inasisitiza umuhimu wa kuzingatiwa amani na kujiweka mbali na dhulma pamoja na vitendo vya utumiaji nguvu. Huku akisisitiza kwamba vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu vina jukumu kubwa katika kutetea na kulinda dini hii tukufu, mwakilishi huyo wa Lebanon katika tamasha la magazeti na mashirika ya habari la mjini Tehran amesema kwamba jukumu hilo haliwezi kutimia kwa kutolewa nara tu bali nchi za Kiislamu zinapasa kufanya jitihada maradufu kwa madhumuni ya kushirikiana katika kutoa mtazamo halisi wa mafundisho ya dini ya Kiislamu. Ameendelea kusema kuwa, Uislamu si dini ya ugaidi na utumiaji mabavu bali ni dini iliyostaarabika na kwa madhumuni ya kumuelekeza mwanadamu katika ukamilifu. Khudhar amegusia nafasi muhimu ya Iran na Lebanon katika kuuarifisha Uislamu na mafundisho yake aali, na kusema kuwa, nchi mbili hizi zina ustaarabu na historia inayong'ara na kwamba hivi sasa zinatekeleza jukumu kubwa la kueneza Uislamu halisi ulimwenguni. Akijibu swali la mwandishi wa IQNA kuhusiana na iwapo vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu vimezembea katika ufikishaji ujumbe halisi wa Uislamu, katika kukabiliana na hujuma ya nchi za Magharibi, Khudhar amesema kuwa jambo hilo halithibiti kuhusian na vyombo vya habari vya nchi zote za Kiislamu kwa sababu kuna baadhi ambavyo vinatekeleza majukumu na nyadhifa zao kwa namna nzuri na ya kuridhisha kabisa. Akiashiria ugaidi unaotekelezwa na nchi mbili za Marekani na Israel katika nchi za Kiislamu, mwakilishi huyo wa Lebanon amesisitiza kwamba nchi mbili hizo ndizo maadui wakubwa wa Uislamu. Amesema, bila shaka kuenea kwa Uislamu ulimwengu kunazikasirisha mno nchi hizo na hivyo kuzifanya zitumie mbinu tofauti katika kukabiliana na dini hii tukufu. Khudhar Majid ameashiria nafasi ya nchi yake Lebanon katika kueneza Uislamu na kusema kuwa, pamoja na kuwa nchi hiyo ni ndogo lakini ina magazeti mengi sana ya kidini yakiwemo ya Kikristo na Kiislamu, ambayo yanatekeleza shughuli zao kwa ajili ya kuarifisha mafundisho ya dini hizo kwa wasiokuwa wafuasi wake. Tamasha la wiki moja la magazeti na mashirika ya habari la mjini Tehran limemalizika leo Jumamosi. 322828
captcha