Mahdi Mustafawi, Mshauri wa Rais na Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametembelea kituo cha nyaraka za maandishi ya mkono cha Sanaa, mji mkuu wa Yemen.
Shirika la habari la nchi hiyo Saba limesema kuwa katika mahojiano yake na shirika hilo, Mustafawi amesema kuwa kituo hicho ni moja ya vituo muhimu vya kuhifadhi urithi na utamaduni wa Kiislamu na kuongeza kuwa, katika kituo hicho kuna baadhi ya nyaraka za kipekee zisizopatikana kwingineko katika ulimwengu wa Kiislamu. Huku akisistiza kwamba utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu unakidhi mahitaji yote ya jamii ya mwanadamu, Mustafawi ameongeza kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuhifadhiwa athari hizo za thamani, na kuwashukuru wakuu wa kituo hicho cha Sanaa kwa kufanya juhudi za kuzilinda athari hizo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameelezea matumaini yake kwamba kituo hicho kitaanzisha mawasiliano na vituo vingine vya Kiislamu ili kuwanufaisha Waislamu wote duniani kwa utajiri wake huo.
Tunakumbusha hapa kwamba, Mustafawi ameuongoza ujumbe wa kiutamaduni nchini Yemen kwa lengo la kuhudhuria sherehe za kufunguliwa rasmi Msikiti na Chuo Kikuu cha Qur’ani cha as-Swaleh. 324294