Alchin Husseiniev, Mkuu wa kitengo cha kimataifa cha shirika la habari la Trend la nchini Azerbaijan, ambaye ni mwakilishi wa nchi hiyo katika Tamasha la 15 la Kimataifa la Magazeti la Mashirika ya Habari la mjini Tehran amesema katika mahojiano yake maalumu na mwandishi wa Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa IQNA kwamba, maadui wa Magharibi kila siku huimarisha hujuma yao dhidi ya Uislamu. Amesema, kwa kuendesha vitendo vya dharau kama vile kuchora vikatuni vya matusi dhidi ya Mtume Mtukufu (saw) na thamani za Kiislamu, maadui hao wa Magharibi wanafanya kila wawezalo ili kuzuia kuenea kwa Uislamu katika nchi za Magharibi. Huku akisistiza kuwa kinyume na wanavyotarajia maadui wa Uislamu, hujuma yao dhidi ya dini hii imeifanya kuenea hata zaidi katika nchi za Magharibi, Husseiniev ameongeza kuwa katika miaka iliyopita, Wamagharibi walikuwa na habari chache sana kuhusiana na Uislamu na Waislamu, lakini kwamba mtazamo wao huo umebadilika sana kutokana na juhudi zinazofanywa na nchi za Kiislamu za kueneza Uislamu pamoja na kufanya maonyesho na matamasha mbalimbali yenye maudhui ya Uislamu na Waislamu. Husseiniev amesisitiza juu ya umuhimu wa nchi za Kiislamu kubainisha Uislamu halisi kwa Wamagharibi na kisha kuwaarifishia mafundisho ya Kiislamu kwa lugha nyepesi na inayofahamika na wote. Mwakilishi huyo wa Azerbaijan katika maonyesho yaliyotajwa ya magazeti na mashirika ya habari amesisitiza kwamba, kuchapishwa kwa vikatuni vinavyomdhihaki Mtume na thamani za Kiislamu katika baadhi ya magazeti ya Ulaya kunathibitisha wazi kutokuwa na utamaduni wakuu wa magazeti hayo na kuwataka Waislamu wasilipize kisasi bali watumie njia zinazofahamika kiutamaduni kama vile za kuandaa matamasha na maonyesho ya kimataifa ili kuwafahamisha watu kama hao kwamba kueneza propaganda kama hizo dhidi ya Uislamu hakuna maslahi kwa kundi lolote lile la kidini. Akizungumzia njama ya Wamagharibi ya kufungamanisha Uislamu na ugaidi, Husseiniev amesisitiza kwamba, masuala hayo mawili kamwe hayawezi kufananishwa wala kufungamanishwa. Amesema, inashangaza kuona kwamba makundi ya Kikristo katika nchi za Ireland na Hispania yanatekeleza vitendo vya ugaidi ulio wazi lakini vyombo vya habari vya Magharibi havithubuti kuyaita makundi hayo kuwa ni ya kigaidi. 324712