IQNA

14:30 - November 29, 2008
Habari ID: 1713840

Picha ya kupeana mikono Sheikh wa al Azhar na Shimon Peres yazusha makelele mengi

Picha inayomuonyesha Sheikh wa Chuo Kikuu cha al Azhar Muhammad Sayyid Tantawi na Rais wa utawala ghasibu wa Israel Shimon Peres katika mkutano uliofanyika hivi karibuni katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York imezusha malalamiko na lawama nyingi za wabunge wa Misri.

Picha hiyo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza Alkhamisi ya wiki hii katika vyombo vya habari vya Misri.
Mwakilishi wa Bunge la Misri Hamdi Hassan ametoa taarifa akisema kuwa kitendo cha Sheikh wa al Azhar cha kumpa mkono Shimon Peres ni kuwadhalilisha wananchi wa Misri, nchi za Kiarabu na za Kiislamu na vilevile mashahidi wote wa Ukanda wa Gaza na Palestina kwa ujumla.
Taarifa hiyo imeongeza kwamba: Sheikh Muhammad Tantawi amepeana mkono na Rais wa utawala ghasibu wa Israel huku akitabasamu wakati utawala huo ukiendelea kufunga vivuko vyote na kutoka na kuingia Gaza na wanananchi wa eneo hilo wakiwa katika mzingiro wa utawala huo.
Taarifa ya Hamdi Hassan imeyataka makundi na vyama vyote vya siasa vya Misri na wananchi kufanya maandamano makubwa ya kutaka kung’olewa madarakani Sheikh wa Chuo Kikuu cha al Azhar.
Mbunge huyo wa Misri amemtaka pia Sheikh Tantawi kuwaomba radhi Waislamu wote kwa kitendo hicho cha aibu na kuchukua msimamo madhubuti katika kutetea mapambano ya wananchi wa Palestina hususan wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mkutano wa kimataifa wa Mazungumzo Kati ya Dini Mbalimbali ulifanyika tarehe 12 na 13 mwezi huu wa Novemba mjini New York Marekani. Mkutano huo ulitayarishwa na Saudi Arabia ambayo imekosolewa sana na Waislamu kote duniani kwa kumwalika Rais wa utawala katili wa Israel Shimon Peres na kiongozi anayeondoka wa Marekani George W. Bush. 326840

captcha