IQNA

Kuwa macho kwa Waislamu katika ibada ya Hija kutazuia fitina za kimadhehebu.

14:37 - November 29, 2008
Habari ID: 1713847
Wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu wanaweza kuzuia fitina za kimadhehebu na hitilafu zinazodhuru maslahi ya Kiislamu kwa kuwa macho zaidi wakati wa kutekeleza ibada ya Hija.
Hayo yamesemwa na mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia Hassan Saffar ambaye pia ni Imamu wa Ijumaa wa eneo la Qatif. Shekh Saffar amesema kuwa wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu wanawajibika kudhihirisha sura sahihi ya Uislamu kwa walimwengu.
Sheikh Hassan Saffar amesema kuwa nchi zote za Kiislamu zinapasa kutoa kipaumbele kwa umoja na mshikamano wa Kiislamu hususan wakati huu ambapo maadui wa dini hiyo wanafanya njama za kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya Waislamu.
Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameashiria mwenendo mbaya wa makundi ya kisalafi na Kiwahabi dhidi ya mahujaji wa Kishia hususan mahujaji hao wanapozuru haram ya Mtume Muhammad SAW na makaburi ya Maimamu wajukuu zake katika eneo la Baqi’ na akasema: Makundi yenye misimamo mikali ya Kiwahabi yanakutambua kuzuru kaburi la Bwana Mtume Muhammad SAW na Masahaba zake katika eneo la Baqi’ kwa ajili ya kupata baraka kuwa ni bidaa na yanavunjia heshima itikadi za ibada zao. Amesema kuwa vitendo hivyo vya Masalafi vinakinzana na sheria za Kiislamu na vinatoa picha mbaya kuhusu jamii ya Saudi Arabia.
Sheikh Hassan Saffar amesema kuwa hii leo ulimwengu wa Uislamu unakabiliwa na makundi yenye chuki za kimadhehebu na kwa msingi huo Waislamu wanapasa kuwa macho wakati wa kutekeleza ibada ya Hija na kujiepusha na baadhi ya amali zinazoweza kuzusha fitina na hitilafu.
Mwanazuoni huyo ameashiria pia nafasi adhimu ya Makka na Madina katika nyoyo za Waislamu na akasema kuwa, Mwenyezi Mungu (sw) ameijaalia al Kaaba kuwa kibla cha Waislamu wote na kila mwaka umati mkubwa wa Waislamu huelekea Makka na Madina kutekeleza amali za Hija. 327180
captcha