Hayo yamesemwa na Prof. Mohsen Reza Haidari mhadhiri katika Chuo cha Udaktari cha Baqiyatullah nchini India. Katika mahojiano maalumu na IQNA, Prof Haidar amesema kuwa: "Kutumia intaneti na kuanzisha mitandao ya lugha mbalimbali kama vile, Kihispania, Kifaransa na Kichina pamoja na kuanzisha jumuiya za wanachuo na wahadhiri Waislamu na waandishi vitabu kuhusu Uislamu ni njia muafaka ya kuuarifisha Uislamu halisi kwa walimwengu".
Ameashiria makala yake iliyojadili kuhusu mtandao wa intaneti wa www.al-islam.org katika kongamano la kimataifa la wanachuo Waislamu lililofanyika hapa Tehran na kusema kuwa: 'Mtandao huo ulianzishwa miaka 12 iliyopita na kundi moja la Waislamu kutoka mataifa mbalimbali kwa lugha za Kiingereza, Kiarabu, Kiurdu, Kihispania na Kitaliano".
Prof. Heidar amesema, mtandao huo unatembelewa na watu wengi kutoka Marekani na una zaidi ya vitabu elfu mbili kwa lugha mbalimbali. Amesema, vitabu hivyo vimeandikwa na wasomi kama vile Imam Khomeini, Shahid Mutahari na Allamah Amini mbali na kuwepo vitabu kama vile Nahjul Balagha na Sahifa Sajaddiya.
Akiendelea na nasaha zake, amesema kipindi cha uanafunzi ndio zama bora zaidi za kutumia intaneti. Ameashiria midahalo ya intaneti kati ya wanachuo Waislamu na Wakristo kwa lengo la kuuarifisha Uislamu halisi. Prof. Heidar amesema kuwa kutusiwa matukufu ya Waislamu ni njama inayotekelezwa na Wazayuni kwa lengo la kuiharibu sura ya Uislamu ulimwenguni na kuzuia kuenea Uislamu katika nchi za Magharibi.
Amesema, hitilafu ndogo ndogo miongoni mwa Waislamu zinazushwa na kukuzwa na maadui wa Uislamu. Amesema, mwamko miongoni mwa wanachuo wa Kiislamu katika vyuo vikuu na kuenezwa mwamko huo katika jamii kutatoa mchango mkubwa katika kuvunja njama za maadui za kuvuruga umoja wa Kiislamu.
327303