Rais wa Yemen amesema Ummah wa Kiislamu unapaswa kufuata mafunzo na thamani za Hija, yaani umoja, mshikamano, udugu na kuheshimiana.
Kwa mujibu wa gazeti la Saba la Yemen, Rais Abdullah Saleh ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Idul Adh'ha na kuongeza kuwa: "Kufuata mafunzo ya kimsingi ya Hija ni jambo la lazimwa iwapo Waislamu wanataka kustawi na kukabiliana na changamoto zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu" .
Ameelezea wasi wasi wake kuhusu mzingiro dhidi ya Wapalestina waliodhulumiwa katika Ukanda wa Ghaza na kulaani vikali kimya cha kuaibisha cha jamii ya kimataifa kuhusiana na kadhia hiyo. Ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kushindwa kuwanusuru wakaazi wa Ghaza wakiwemo wanawake na watoto ambao wanakabiliwa na mateso ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.
"Umoja wa Mataifa unapaswa kutoa misaada ya kibinaadamu na kutekeleza majukumu yake katika kuhitimisha hali hii ya kusikitisha ya Ukanda wa Ghaza na vile vile kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel kusitisha mgogoro huu", amesema Rais Abdullah Saleh.
Rais wa Yemen amemaliza kwa kutoa wito kwa Waislamu kutumia Idul Adh'ha kama fursa ya kueneza mwenendo wa kuaminiana na kupendana miongoni mwa Waislamu kote duniani. 331587