Kwa mujibu wa tovuti ya www.alqubanchi.com, Hujjatul Islam wal Muslimeen Swadr ad-Deen Qubanchi, Imam wa swala ya Ijumaa ya mji mtakatifu wa Najaf amesema katika hotuba ya swala ya Ijumaa kwamba, askari wa utawala haramu wa Israel wamezingira na kuwatesa Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza huku Waislamu wakiwa wamenyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana katika kukabiliana na jinai za utawala huo. Amesema, katika hali ya hivi sasa, Waislamu katika nchi za Kiislamu wanakabiliwa na wimbi kubwa la hujuma ya fitina na mfarakano na kwamba, makundi ya kukufurisha Waislamu yanafanya juhudi za kupotosha fikra za Waislamu na hasa tabaka la vijana na hivyo kufuta kabisa utambulisho wao halisi wa Kiislamu. Imam wa swala ya Ijumaa ya Najaf mwishoni mwa hotuba yake amewatakia idi njema Waislamu wote ulimwenguni na kusisitiza kwamba Wairaki ni Waislamu ambao wanataka kuhifadhiwa na kulindwa kwa haki zao zote za kidini na kisiasa.332170