IQNA

Hitilafu za kimadhehebu isiwe sababu ya kuwanyima watu haki zao za kiraia

18:37 - December 15, 2008
Habari ID: 1719536
Mazungumzo na ushirikiano kati ya wafuasi wa madhehebu na makabila mbalimbali unaimarisha nukta za pamoja za pande hizo na kudhoofisha mielekeo ya kupindukia mipaka katika jamii za Kiislamu. Hayo yamesemwa na Muhammad al-Mahfudh, mtafiti na msomi wa Kiislamu kutoka nchini Saudi Arabia katika kikao cha ‘Mashirika ya Kiislamu na changamoto za mirengo’ kilichofanyika huko nchini Bahrain.
Amesema, hitilafu za kimadhehebu na kifikra haipasi kuchukuliwa kuwa kizuizi cha wananchi kudhaminiwa haki zao za kiraia. Amesema kwamba, tatizo kubwa la baadhi ya nchi za Kiislamu ni kukubali fikra na madhehebu mbalimbali yasiyokubalika wala kukaribishwa na serikali za nchi hizo. Al-Mahfudh amesema kuwa wingi wa madhehebu na fikra ni jambo la kawaida kabisa na kwamba jambo lisilo la kawaida ni serikali za Kiislamu kubuni katiba na sheria zinazozuia jambo hilo. Washiriki wa kikao hicho cha Bahrain wametoa taarifa mwishoni mwa kikao chao wakitaka serikali za Kiislamu zibuni sheria ambazo zitawaadhibu watu na makundi yanayobagua na kupinga wafuasi wa madhehebu nyingine zisizokuwa zao. Washiriki pia wamezitaka serikali za Kiislamu kubuni sheria ambazo zitaruhusu kufundishwa mashuleni masomo yanayokubaliana na fikra pamoja na itikadi za madhehebu mbalimbali za Kiislamu na kuzuia kufundishwa mambo yanayochochea hisia za kimadhehebu na kimirengo katika nchi za Kiislamu na badala yake kuimarishwa fikra za udugu na umoja. Kikao hicho kimefanyika kwa ajili ya kuchunguza changamoto na matatizo ya kimirengo na kimadhehebu na nafasi ya mashirika na taasisi za Kiislamu katika uwanja huo, kwa mnasaba wa kuadimishwa mwaka wa 60 wa kutangazwa azimio la kimataifa la haki za binadamu. 333596
captcha