IQNA

Azimio lisilo la uwajibikaji la Baraza la Usalama kuhusiana na Gaza

9:04 - December 29, 2008
Habari ID: 1724041
Muhammad Jasim as-Swaqr, Spika wa Bunge la Waarabu amesema kuwa hatua ya Baraza la Usalama ya kutoa azimio lisilo na ulazima wa kutekelezwa kwa ajili ya kusimamishwa mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia huko katika Ukanda wa Gaza, ni jambo lisilo na maana na linalokaririwa mara kwa mara.
Amesema, hatua kama hiyo inachukuliwa kwa lengo la kuupa utawala haramu wa Israel mwanya wa kuendelea kutekeleza jinai na unyama wake dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi. Shirika rasmi la habari la Kuweit KUNA limefanya mazungumzo na Jasim ambapo limemnukuu akisema kuwa, mashambulio ya anga yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel ni ishara ya wazi ya utambulisho wa utawala huo na kutoheshimu kwake sheria za kimataifa kuhusiana na suala la Palestina. Amezitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, taasisi za kimataifa na kieneo pamoja na wabunge wa nchi za Kiarabu kufanya juhudi za kusimamisha mara moja mashambulio hayo ya kinyama yanayofanywa na utawala unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu na wakati huohuo kufikisha misaada ya dharura kwa wakazi wa Gaza wanaokabiliwa na hali ngumu ya uhaba wa chakula kutokana na mzingiro wa kidhulma unaotekelezwa dhidi ya ukanda huo na utawala wa Tel Aviv.
Muhammad Jasim pia amewataka maspika wa mabunge ya nchi za Kiarabu kufanya kikao cha dharura mjini Cairo Misri, makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ili kuchunguza jinai za utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na vilevile kubadilishana mawazo kuhusiana na hali nzima na hatari ya eneo hilo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi usiku lilifanya kikao cha dharura kwa ombi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ili kuchunguza hali ya kusikitisha ya Gaza, lakini mwishowe lilitoa tu azimio lisilo na ulazima wa kutekelezwa, la kuutaka utawala wa Tel Aviv kusimamisha mashambulio yake huko Gaza. Hilo lilitokana na upinzani mkali wa Marekani dhidi ya kutolewa azimio lolote la kuulazimisha utawala huo kusimamisha mashambulio hayo ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia. 339641
captcha