Mashirika na makundi hayo ya Kiislamu yamesikitishwa sana na kimya hicho na hata ushirikiano wa baadhi ya serikali hizo na utawala wa kibaguzi wa Israel katika utekelezaji wake wa mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Shakhsia wa Kidini na Kiislamu ambao wamezungumzia jambo hilo wamesema kuwa, kimya cha nchi za Kiislamu kiinaupa kichwa utawala wa Israel kuendelea kutekeleza mauaji na jinai dhidi ya Wapalestina katika hali ambayo zinatakiwa kushirikiana na wananchi Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu kwa lengo la kukabiliana na jinai hizo.
Yusuf Qardhawi, Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu amezitaka nchi za Misri na Saudi Arabia pamoja na jamii ya kimataifa kuchukua msimamo wa kimantiki na kuzuia kuendelea kutekelezwa kwa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, pia imetoa taarifa ikilaani vikali mashambulio hayo ambayo yamefanyika sambamba na safari ya Tzipi Livni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Utawala haramu wa Israel nchini Misri na kusema kuwa, msimamo wa nchi za Kiarabu wa kuunga mkono waziwazi utawala wa Israel kuhusiana na suala la Palestina ni aibu kubwa kwa umma wa Kiarabu na Kiislamu.
Hizbullah imesema kuwa, hujuma ya kijeshi ya Wazayuni huko katika Ukanda wa Gaza ni jinai za kivita na mauji ya umati, na imezitaka nchi za Kiislamu kutumia uwezo wao wote kwa ajili ya kukabiliana na unyama huo wa Wazayuni. Taarifa hiyo pia imesisitiza kwamba kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na uchokozi wa utawala wa Israel ndicho kinachoupelekea utawala huo kumea pembe na kuendelea kuwakandamiza kinyama raia Wapalestina wasio na hatia. 339447