IQNA

12:35 - January 04, 2009
Habari ID: 1724470

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu maafa ya Gaza

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe muhimu kuhusu maafa na mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Gaza akilaani jinai hiyo na kutangaza Jumatatu ya wiki hii kuwa ni siku ya maombolezo ya taifa nchini Iran.

Ayatullah Khamenei amelaani himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za utawala ghasibu wa Israel na akasema: Kimya cha jumuiya na taasisi za kimataifa na pia baadhi ya nchi za Kiarabu, kimetayarisha uwanja wa kufanyika jinai hiyo ya mauaji ya umati dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
انا لله و انا اليه راجعون
Hakika sisi ni wa Allah na kwa hakika tutarejea Kwake.
Jinai kubwa mno za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kuuliwa kwa umati mamia ya wanaume, wanawake na watoto madhulumu, kwa mara nyingine kumeondoa pazia lililofunika sura ya kupenda kufyonza damu za watu ya mbwa mwitu wa Kizayuni sura ambayo ilikuwa haionekani vizuri katika miaka ya hivi karibuni na kutangaza wazi hatari ya kuwepo kafiri huyo mpenda vita katika kitovu cha ardhi za umma wa Kiislamu mbele ya watu walioghafilika na wasiojali.
Msiba wa tukio hili la kutisha ni mkubwa mno na unaomuumiza mno kila Muislamu bali kila mwanadaamu mwenye utu na heshima katika kila kona ya dunia. Pamoja na hayo, msiba mkubwa zaidi ni kimya cha kushajiisha maadui cha baadhi ya tawala za Kiarabu zinazodai ni za Kiislamu. Kuna msiba gani mkubwa zaidi ya huu wa tawala za Waislamu ambazo zinapaswa kuwalinda wananchi madhulumu wa Ghaza mbele ya utawala ghasibu na kafiri unaopenda vita wa Kizayuni, lakini badala yake zinafanya mambo ambayo yamewapelekea viongozi watenda jinai za Kizayuni kuwafedhehesha hadharani kwa kuwatangaza kuwa wanaunga mkono na walishiriki katika kuratibu jinai hizo kubwa zinazoendelea Ukanda wa Ghaza.
Viongozi wa nchi hizo (za Kiarabu) watakwenda kumjibu nini Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)? Wana majibu gani ya kuwapa wananchi wao ambao kwa yakini wamo katika kuomboleza maafa ya Ghaza? Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba nyoyo za wananchi wa Misri, Jordan na nchi nyingine za Kiislamu zinavuja damu kutokana na mauaji yanayowakabili wananchi wa Ghaza tena baada ya kupitisha kipindi kirefu cha kuzingirwa na kunyimwa chakula na madawa.
Serikali yenye kutenda jinai ya Bush inashiriki katika jinai hiyo kubwa katika siku za mwisho za utawala wake uliojaa aibu. Jinai hiyo inalifanya faili la utawala wa Marekani kuzidi kuwa jeusi na kwamba faili la uhalifu wake ambalo linawafanya viongozi wa utawala huo kuhesabiwa kuwa watenda jinai za kivita, linazidi kuwa kubwa. Aidha kutokana na kutojali kwao na pengine kushiriki katika jinai hiyo kubwa, tawala za Ulaya nazo kwa mara nyingine zimethibitisha uongo wa madai yao ya kutetea haki za binaadamu na zimethibitisha kushiriki kwao katika vita dhidi ya Uislamu na Waislamu. Swali langu kwa maulamaa na viongozi wa kidini wa ulimwengu wa Kiarabu na wakuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri ni hili kwamba je wakati haujafika wa kuhisi hatari inayoukabili Uislamu na Waislamu? Je wakati haujafika wa kukuwajibikieni kukataza maovu na kusema neno la haki mbele ya kiongozi muovu?
Je tukio gani jingine lililo wazi zaidi, kushinda yale yanayotokea Ghaza Palestina, linaloweza kuonyesha ushirikiano baina ya kafiri mpenda vita na wanafiki katika umma wa Kiislamu katika vita vya kuwaangamiza Waislamu? Mnasubiri tukio gani jingine la kukuwajibisheni kusimama kidete na kupambana na dhulma?
Swali langu kwa duru za wasomi katika ulimwengu wa Kiislamu hususan ulimwengu wa Kiarabu ni kwamba, hadi lini zitaendelea kutojali majukumu yao? Je mashirika ya haki za binaadamu yanahisi kuna kashfa gani kubwa zaidi ya hii ya hivi sasa ambayo imezikumba nchi za Magharibi na Baraza eti la Usalama la Umoja wa Mataifa?
Wapiganaji jihadi wote wa Palestina na waumini wote katika ulimwengu wa Kiislamu wana jukumu la kuwalinda na kuwatetea wanawake, watoto wadogo na wanaume wasio na ulinzi huko Ghaza kwa kila njia inayowezekana na yeyote atakayeuawa katika kujihami huko kutakatifu atakuwa ameuawa shahidi na atapata matumaini ya kufufuliwa katika safu za mashahidi wa Badri na Uhud mbele ya Mtume Muhammad SAW.
Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ina jukumu la kutekeleza wajibu wake wa kihistoria katika wakati huu mgumu na inapaswa kuunda kambi iliyoshikamana isiyo na woga wala pupa ili iweze kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Mataifa ya Kiislamu yanapaswa kuuadhibu utawala wa Kizayuni. Viongozi wa utawala huo ghasibu lazima wafikishwe mbele ya sheria mmoja baada ya mwingine kutokana na uhalifu wao wa kutenda jinai na kuuzingira kwa muda mrefu Ukanda wa Ghaza.
Mataifa ya Kiislamu yanaweza kufanikisha wajibu huo kwa msimamo na azma yao thabiti ambapo jukumu la wanasiasa, maulamaa na wasomi katika kipindi hiki nyeti ni kubwa mno ikilinganishwna wengine.
Natumia fursa hii kutangaza siku ya Jumatatu (Disemba 29, 2008) kuwa siku ya maombolezo ya maafa ya Ghaza na ninatoa mwito kwa viongozi nchini (Iran) kutekeleza majukumu yao ya kukabiliana na tukio hili la kuhuzunisha.
وَ سَيعلَمُ ‌الذين ظَلَموا اَیّ مُنقلبٍ یَنقلبون.
Na wanaodhulumu watakujajua mgeuko gani watakaogeuka. (26:227).
Sayyid Ali Khamenei
8 Dei 1387
29 Dhilhaji 1429.
339638
captcha