Iwapo serikali ya Kiislamu na huru ya Palestina itaundwa katika Mashariki ya Kati, utawala ghasibu wa Israel utadhoofika sana, ni kutokana na ukweli huo ndipo utawala huo ukatumia kila mbinu na njama kwa ajili ya kubuni dola la Kiyahudi lenye nguvu katika eneo hili.
Hayo yamesemwa na Swaleh Fahs, mwakilishi wa chama cha Amal cha nchini Lebanon nchini Iran alipokuwa akizungumza na shirika la IQNA. Amesema kuwa kamwe utawala haramu wa Israel haukubaliani na fikra ya kubuniwa taifa huru la Palestina kwa sababu kwa mujibu wa imani ya Mayahudi, Palestina ni ardhi zilizoahidiwa kwa kabila la Mayahudi na kwamba Mayahudi wote wa ulimwengu wanapasa kukusanyika na kuishi katika ardhi hizo. Amesema, kuwa Israel ambayo imebuniwa kidhulma kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu inadumisha mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina kwa lengo la kujipanua na kuzuia kuundwa kwa taifa huru la Kiislamu la Wapalestina katika eneo hili nyeti la Mashariki ya Kati. Fahs amesema kuwa, utawala haramu wa Israel unakaribia katika siku zake za mwisho kwa sababu kila unyama ambao umekuwa ukiutekeleza dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Palestina haujausaidia kumaliza mapambano ya wananchi hao shupavu wasio na silaha yoyote isipokuwa imani yao kwa Mwenyezi Mungu.
Mwakilishi huyo wa amal nchini Iran amesisitiza kwamba, kushiriki kwa Wapalestina wote katika mapambano dhidi ya mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na utawala wa Israel dhidi yao ni ishara ya wazi kwamba intafadha yao imefanikiwa kushinda njama za utawala huo na waungaji mkono wake wa Magharibi. Fahs amesikitishwa sana na uungaji mkono pamoja na ushirikiano wa nchi za Kiarabu dhidi ya ndugu zao Waarabu na kusema kuwa Israel inatumia ushirikiano huo kwa lengo la kuwakandamiza Wapalestina kwa sababu unafahamu vyema kwamba nguvu yake tu bila ya kutegemea ushirikiano huo haiwezi hata kidogo kuyashinda mapambano ya wananchi shupavu wa Palestina. Amesema, nchi za Kiarabu zinashirikiana na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina kutokana na kuiogopa Marekani na kwa ajili ya kulinda maslahi yao kwa madhara ya ulimwengu mzima wa Kiislamu. 339508