Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana huko katika mji mkuu wa Ufaransa Paris, kwa lengo la kujadili mashambulio ya anga yanayofanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuuliwa raia wasio na hatia katika ukanda huo.
Bernard Kouchner, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ambaye nchi yake ndiyo inayoshikilia kwa sasa uwenyekiti wa Umoja wa Ulaya, amenukuliwa akidai kwamba, kuongezeka kwa mashambulio hayo ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza kumezitia wasiwasi mkubwa nchi za Ulaya. Amesema, Umoja wa Ulaya unafanya juhudi za kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kumaliza kwa amani mgogoro wa Gaza na hatimaye kufungua njia za kuingizwa katika ukanda huo misaada ya dharura yakiwemo maji, madawa na chakula. Akiashiria kuuawa kwa zaidi ya Wapalestina 365 katika mashambulio ya siku nne zilizopita, Waziri huyo wa Ufaransa ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kusimamisha mara moja mashambulio yake dhidi ya raia wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa pia amenukuliwa akidai kwamba, nchi hiyo ni mdhamini mkubwa wa misaada ya kiuchumi na kibinadamu wa wakazi wa Ukanda wa Gaza na kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kukidhi mahitaji yote ya dharura ya wakazi wa Gaza. 340843