Chama cha kisoshalisti cha Italia PSI kimemtaka Rais Giorgio Napolitano wa nchi hiyo kusimamisha kwa muda mikataba yote ya kijeshi iliyotiwa saini kati ya nchi hiyo na utawala haramu wa Israel kutokana na mashambulio yake ya kinyama inayoyatekeleza dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Jacob Venier, Mkuu wa Uhusiano wa Kigeni wa chama hicho amesema kuwa kwa mujibu wa sheria za Italia, uhusiano wa kijeshi unapaswa kusimamishwa na nchi yoyote ile inayotekeleza jinai za kivita, na kwamba sheria hizo hivi sasa zinahusu uhusiano wa nchi hiyo na utawala haramu wa Israel.
Walter Veltron, Kiongozi wa chama cha Uhuru cha Italia, ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini humo pia ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kusimamisha mara moja mauaji yanayotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, akisema kuwa hatua ambazo hadi sasa zimechukuliwa katika uwanja huo hazitoshi kabisa. Amesema kuwa amani na suluhu haiwezi kupatikana katika Mashariki ya Kati kupitia mauaji ya umati yanayotekelezwa na Israel dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina na kwamba njia pekee ya kuleta amani ya kudumu katika eneo ni kuheshimiwa haki za nchi zote. Chama cha Kijani cha Italia pia kimetaka kusimamishwa mara moja mashambulio na mauaji yanayotekelezwa na Israel huko katika Ukanda wa Gaza na kuitaka jamii ya kimatiafa kuingilia kati ili kumaliza mgogoro wa ukanda huo. 340890