Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusitisha mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel yanayoendelea kwa siku ya sita mfululizo. Nchi za Kiarabu zimelitaka Baraza la Usalama kutoa azimio linaloilazimisha Israel kusimamisha mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina, kukomesha mzingiro wa Gaza na siasa za kuwatesa kwa umati Wapalestina na pia kutoa himaya ya kimataifa kwa taifa hilo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Amr Mussa amesema kuwa kikao hicho pia kimejadili masuala mbalimbali ya Palestina, umoja wa makundi ya taifa hilo na wito uliotolewa na nchi za Qatar na Syria wa kuitisha mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu.
Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aliwasilisha katika kikao hicho ripoti kuhusu mitazamo ya nchi wanachama katika ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi juu ya jinsi ya kukabiliana na mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Wawakilishi wa nchi hizo walikutana tarehe 29 Disemba katika mji mkuu wa Oman, Mascut. 341703