Hassan as-Swaffar, Imam wa Swala ya Ijumaa ya eneo la Qatif nchini Saudi Arabia amesema kuwa kuhuishwa kwa nara na vielelezo vya Imam Hussein (as) na kuomboleza kifo chake katika siku za mwezi mtukufu wa Muharram kunanasibiana na kuoana na misingi ya Qur'ani Tukufu pamoja na thamani za kiutu.
Akizungumza katika msikiti wa Sheikh Mubarak, Sheikh Hassan as-Swaffar amesema kwamba, matukio ya Ashura na kuuawa shahidi Imam Hussein na wafuasi wake ni jinai kubwa zaidi kuwahi kufanywa katika historia nzima ya mwanadamu, na kwamba kuhuishwa kwa matukio hayo kwa ajili ya kupata ibra kutokana nayo ni jambo lisilopingana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu wala thamani za kibinadamu. Amesema, mafundisho ya dini zote za mbinguni yanasisitiza juu ya audilifu na kupinga dhulma na uonevu dhidi ya binadamu na hilo ni jambo ambalo linasisitizwa na kutiliwa mkazo na misingi pamoja na sheria za haki za binadamu. Amesema, upotofu wa kifikra ni jinai na dhulma kubwa zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya mwanadamu katika kipindi chote cha historia na kuongeza kuwa, mapambano ya Karbala yalianza kwa lengo la kupambana na upotofu huo pamoja na wa kiitikadi. Amesema, kwa masikitiko makubwa kuna baadhi ya taasisi potofu na zenye taasubi ambazo zinafanya njama za kuyaweka mataifa mbalimbali katika hali hiyo ya upotofu wa kudumu. Hassan as-Swaffar hatimaye amelaani vikali unyama na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko katika Ukanda wa Gaza dhidi ya wananchi wasio na hatia na kuwataka watawala wa nchi za Kiarabu na wa nchi nyingine za ulimwengu kufanya juhudi za kukomesha mara moja mauaji hayo. 342433