IQNA

Kuanza mpango wa misaada ya kibinadamu wa OIC kwa ajili ya wakazi wa Gaza

16:15 - January 06, 2009
Habari ID: 1728143
Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) imezindua mpango wa kutuma misaada ya kibinadamu kwa raia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Ekmeleddin Ihsanoglu amesema kuwa mpango huo ulipasishwa katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiislamu uliofanyika hivi karibuni mjini Jeddah, Saudi Arabia kujadili mgogoro wa Gaza.
Amesema kuwa, mpango huo wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza unasimamiwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ikishirikiana na taasisi za kifedha za Kiislamu na jumuiya za kazi za kheri. Mpango huo unajumuisha misaada ya chakula, dawa, nishati na mahitaji mengine muhimu ya watu wa Gaza.
Ihsanoglu amesema kuwa lengo la kutekelezwa mpango huo ni kupunguza mashaka na masaibu yanayowapata wananchi wa Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya kinyama ya askari wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya eneo hilo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameeleza kusikitishwa na kushindwa kwa Baraza la Usalama kusimamisha mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya wananchi wa Gaza na akasema, jumuiya hiyo inafanya jitihada kubwa za kukomesha mashambulizi hayo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na taasisi nyingine za kimataifa za Kiislamu. 344357
captcha