Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Nchi za Kiislamu Isesco limeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuwafikisha watawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutokana na mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala huo dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.
Shirika hilo lenye makao makuu yake mjini Rabat Morocco, limetoa taarifa ikizitaka nchi za ulimwengu wa tatu na vilevile mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, kuwasilisha katika mahakama iliyotajwa faili kamili la jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza. Taarifa hiyo imetaka watawala hao kuandamwa na kusakwa kimataifa na hatimaye kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa kutokana na jinai za kutisha wanazotekeleza huko Gaza. Taarifa ya Isesco imesema kuwa, mbali na kuwashinikiza wakazi milioni moja na nusu wa Gaza kupitia mzingiro wa kidhulma unaoutekelezwa dhidi ya ukanda huo, utawala wa Israel umekuwa ikitekeleza jinai dhidi ya wanawake na watoto kwa kuwaua kwa umati na vilevile kuharibu ovyo mashule, misikiti pamoja na kuyashambulia mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa. Imesema mbali na kutekeleza ugaidi unaodhaminiwa na serikali huko Gaza, watawala wa Israel wamekuwa wakikanyaga wazi haki za kimsingi za binadamu katika ukanda huo. Taasisi hiyo pia imezitaka nchi zote na jumuiya za kimataifa kutuma misaada ya chakula na dawa huko Gaza. 345232