Ignazio La Russa, Waziri wa Ulinzi wa Italia amewataka Waislamu wa nchi hiyo kusimamisha uungaji mkono wao kwa watu wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na hali ngumu kutokana na jinai na mauaji ya umati yanayotekelezwa dhidi yao na utawala haramu wa Israel, na pia kutosimamisha swala katika maeneo ya hadhara nchini humo.
Akiwatuhumu Waislamu wanaonyesha wazi uungaji mkono wao kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza nje ya misikiti na pia kusimamisha swala na kuomba dua ya kunusuriwa wakazi hao wanaokabiliwa na mauaji ya umati kutoka kwa Wazayuni katika maeneo ya hadhara kuwa ni watu wenye misimamo ya kupindukia mipaka, Waziri huyo wa Ulinzi wa Italia amesema kuwa shughuli za watu hao huko Milan zinatosha na kuwaonya Waislamu hao kukoma kufanya ibada ya swala katika maeneo ya hadhara.
Tunakumbusha hapa kwamba, Jumamosi iliyopita, Waislamu wa Italia walikusanyika katika kituo kikuu cha vyombo vya usafiri huko Milan na kuswali swala ya jamaa wakiowambea wenzao huko Gaza wapate kusalimika na mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa dhidi yao na Wazayuni.
Wiki iliyopita pia Waislamu hao walikusanyika mbele ya kanisa kuu la Milan na kutoa nara za kulalamikia mashambulio hayo ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza. Wakiwa mbele ya kanisa hilo waliwaombea dua wenzao wa ukanda huo wapate kuondokana na madhara ya utawala huo wa kibaguzi. 346857