IQNA

Ayatullah Bashir Najafi:

Ulimwengu wa Kiislamu usitosheke na kulaani jinai za Israel kwa maneno matupu

10:43 - January 13, 2009
Habari ID: 1730319
Ayatullah Bashir Najafi ambaye ni mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa kidini wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq amelaani vikali jinai zinazoendelea kufanywa na Wazayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na akawataka viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu na shakhsia wa ulimwengu wa Kiislamu wasitosheke kwa kulaani jinai za Israel kwa maneno matupu.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Ayatullah Sheikh Bashir Najafi katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq imesema kuwa: "Ni wajibu wa kidini na kibinadamu kwa Waislamu wote kuwasaidia kimaada na kimaanawi wananchi wasiokuwa na hatia na wanaodhulumiwa wa Gaza.
Taarifa hiyo imesema: Tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoasisiwa katika kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu kama mfumo ghasibu na wa kivamizi, umemwaga damu ya watu wengi wasiokuwa na hatia na kukanyaga heshima na hadhi ya mwanadamu.
Ayatullah Najafi amesema: Katika mashambulizi yake huko Gaza, Israel inatumia silaha za mauaji ya umati na zilizopigwa marufuku kimataifa kuwaangamiza wakazi wa Gaza na inakiuka sheria za kimataifa zinazosisitiza juu ya kulindwa maisha ya raia.
Ameashiria kuwa wanawake, watoto wadogo, misikiti, mahospitali na shule za Gaza hazikusalimika na mashambulizi hayo ya kinyama ya Wazayuni, na amewataka viongozi wa Kiislamu na watawala wa nchi za Kiarabu kufanya harakati zaidi za kusimamisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na wasitosheke kwa maneno matupu.
Ayatullah Najafi amewataka Waislamu kuwasaidia raia wanaodhulumiwa wa Gaza na kuwaombea dua ya kupata ushindi dhidi ya Wazayuni. 347172
captcha