IQNA

Kuuawa kwa waandishi wa Kiislamu, siasa za vyombo vya habari vya Kizayuni

10:28 - January 15, 2009
Habari ID: 1731170
Utawala haramu wa Israel unalenga na kuwaua kwa makusudi waandishi habari wa nchi za Kiislamu kwa lengo la kuwazuia wasiandike na kupasha habari za kweli kuhusiana na jinai zinazotekelezwa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza, na kuruhusu vyombo vya Kizayuni kufunika jinai za utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Hayo yamesemwa na Muhammad Swaleh Swadigiyan, Mkuu wa Kituo cha Kiarabu cha Utafiti wa Iran, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Mashariki ya Kati. Amesema, vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu vina nafasi muhimu kuhusiana na suala hilo kwa kufichua jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza na kuwafahamisha walimwengu mambo halisi yanayotendeka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Vyombo vya habari vya Kiislamu hadi sasa vimekuwa na nafsi muhimu katika kufichua njama na jinai za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza kwa kuakisi vilivyo matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika ukanda huo tokea utawala haramu wa Israel uanzishe hujuma yake ya kinyama dhidi ya watu wasio na ulinzi katika ukanda huo.
Swadiqiyan amesema kuwa iwapo Waislamu watafuata na kutekeleza vilivyo mafundisho ya Qur’ani Tukufu katika kutetea dini na ardhi zao katika kukabiliana na makafiri, ni wazi kuwa ushindi wa mwisho utakuwa ni wao. Amesisitiza kwamba, kama kungekuwepo na ushirikiano wa kutosha kati ya vituo na taasisi za Kiislamu katika nchi mbalimbali, ni wazi kuwa shughuli zao zingeweza kuzishinikiza serikali za Kiislamu na Kiarabu kukata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel kwa kuwafukuza mabalozi wa utawala huo katika nchi zao. Swadiqiyan amesema kwamba, hadi sasa vituo na wanazuoni wa Kiislamu hawajatekeleza majukumu yao ipaswavyo kuhusiana na suala la Ukanda wa Gaza.
Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati amesifu mapambano ya wanamapambano shupavu wa Hamas katika kukabiliana na hujuma ya Wazayuni na kusema kuwa, licha ya kwamba mashambulio ya kinyama ya utawala huo yameingia katika wiki yake ya tatu lakini hadi sasa hayajaufanya utawala huo kufikia hata sehemu ndogo tu ya malengo yake katika ukanda huo. 347235
captcha