Akizungumza mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliokusanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa, Ayatullah Ahmad Jannati amelaani vikali mauaji ya umati yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wala kinga huko Gaza na kuwashukuru wananchi wa Iran na wengineo ulimwenguni ambao wamekuwa wakifanya maandamano makubwa ya kuwatetea wakazi wa ukanda huo wanaokabiliwa na ukatili mkubwa kutoka kwa watawala wa Israel.
Amesikitishwa mno na uzembe ambao umeonyeshwa na Baraza la Usalama pamoja na watawala wa nchi za Kiarabu kuhusiana na suala hilo. Amesema kuwa azimio lililotolewa hivi karibuni na Baraza la Usalama la kuutaka utawala wa Israel usimamishe mara moja mashambulio yake ya kinyama dhidi ya wakazi wa Gaza halikuwa na uzito wowote kwa sababu halijaweza kusimamisha wala kulaani mashambulio ya mabomu na silaha zilizopigwa marufuku, ikiwemo fosforasi nyeupe, zinazotumiwa na utawala huo katika maeneo ya makazi ya raia na hivyo kuwaua kinyama watu wasio na hatia, wakiwemo watoto wadogo na wanawake.
Hatibu wa Swala wa Ijumaa ya Tehran amesema,Waislamu wana jukumu zito la kuwatetea ndugu zao wanaouawa kwa umati huko Gaza na kwamba inasikitisha kuona kuwa nchi nyingi za Kiislamu zinatawaliwa na watawala wasiofaa ambao wanahodhi madaraka ya nchi hizo kwa madhara ya Waislamu. Ameashiria hatua ya kishujaa iliyochukuliwa hivi karibuni na Venezuela na kusema kuwa inaaibisha kuona kwamba nchi za Kiarabu haziwezi kuchukua hatua kama hiyo ambayo imechukluwa na nchi ambayo yenyewe si ya Kiarabu wala Kiislamu.
Amewaonya watawala wa nchi za Kiarabu kutahadhari siku ambayo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu itawafika. Amesifu mapambano ambayo hadi sasa yameonyeshwa na wapiganaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas na kusema kuwa watawala wa Marekani na Israel hawakutarajia kuona mapambano kama hayo ya kishujaa yakionyeshwa na watu ambao wamekuwa chini ya kila aina ya vikwazo na mzingiro kwa karibu mika miwili, na wasiokuwa na silaha zozote za maana. 349052