Hayo yamesemwa na Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar Shirazi katika mazungumzo ya simu na IQNA.
Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar ameongeza kuwa:"Baada ya kufeli Israel katika vita vya siku 33 dhidi ya Lebanon, Ehud Olmert na chama chake cha Kadima kilikumbwa na matatizo makubwa na ili kufidia matatizo hayo, katika siku za mwisho za utawala wa Bush kulipangwa njama ya kuvamia Ukanda wa Gaza ili kuzidisha uwezekano wa ushindi wa chama hicho kwa kumwaga damu ya raia wakiwemo watoto na wanawake na kwa jina la kupambana na Hamas." Ameongeza kuwa, katika miaka iliyopita, kwa mara kadhaa utawala wa Kizayuni ulitekeleza jinai za kinyama katika maeneo ya Kiislamu na hivi sasa eneo la Gaza liko katika makucha dhalimu ya utawala huo. Amesema ushirikiano wa baadhi ya nchi za kieneo na adui Mzayuni pamoja hiana na usaliti wa viongozi wa nchi hizo kwa Waislamu wa Gaza ni jambo ambalo limeusaidia utawala wa Kizayuni kufikia malengo yake.
Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania amesema kuwa, Utawala wa Kizayuni umetekeleza mauaji ya kimbari ya watoto na wanawake wa Palestina kwa kutumia kisingizo cha kupambana na kuwaagamiza wapiganaji wa Hamas jambo ambalo linafaniyika katika fremu ya ushirikiano wa utawala huo na Marekani. "Kadhia ya Palestina inatumiwa na tawala za Marekani na Israel kama njia ya kuangamiza Uislamu na Waislamu na kuwapokonya uwezo walionao", amesema Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar.
Afisa huyo mwandamizi wa Iran nchini Tanzania amesisitiza kuwa, Utawala haramu wa Israel unatumia mbinu zote chafu kufikia malengo yake na kusema kuwa: "Vita hivi vya umwagaji mkubwa wa damu huko Gaza havijaibuka ghalfa bila mpangilio na wala hii haitakuwa jinai ya mwisho ya Wazayuni katika eneo la Mashariki ya Kati".
Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar ameashiria kushindwa Israel katika vita vya Gaza na kubainisha kuwa: "Pamoja na kwamba Israel imetumia uwezo wake wote wa kijeshi dhidi ya watu walio chini ya mzingiro mkali wa kiuchumi na wanaosumbuliwa na ukosefu wa chakula na madawa na baada ya kupita siku 22 za mashambulizi yasiyo na kikomo, Wazayuni hawajaweza kufikia malengo yao katika hali ambayo utawala huo ulijigamba kuwa ungeliisambaratisha Gaza kwa siku saba za mwanzo wa vita".
Afisa huyo wa utamaduni ameutathmini mpango eti wa amani kati ya Israel na Waarabu kuwa ni hadaa tupu na kuongeza kuwa: "Kwa kuandaa mikutano eti ya amani, kwa upande mmoja adui anakusudia kuingilia mambo ya ndani ya Waislamu na kwa upande wa pili anataka kutumia ujanja ili kuwatumbukiza Waislamu katika migongano ya kimadhehebu na kueneza fitina baina ya makundi ya wanamapambano wa Kiislamu".
Amesema kuwa, Marekani imekuwa ikifuatilia ujanja na njama hizo kwa mkakati mkubwa nchini Lebanon ili kuzusha mifarakano baina ya Waislamu wa madehebu za Shia na Sunni na vile vile baina ya wafuasi wa dini za Kikristo na Kiislamu. "Hata hivyo kutokana na kuwa wanamapambano wa Kiislamu wamechukua tahadhari na wana mafunzo ya kutosha kuhusu njama hizo, adui hajaweza kufanikiwa katika malengo yake", ameongeza afisa huyo.
Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania amesema, kuuawa wanawake, watoto, raia wasio na hatia pamoja na wapigania ukombozi huko Gaza si jambo linalowahusu Waislamu tu bali sasa limebadilika na kuwa suala la wanadamu wote duniani kutokana na jinai za kinyama zinazotekelezwa na Israel. Amesema, Waislamu wanapaswa kuondoa vizingiti vilivyopo katika njia ya wanamapambano wa Gaza ili waweze kutoa jibu la mwisho kwa Israel.
Akiashiria hotuba ya Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran kuhusu kuanza mwenendowa kuangamia Israel amesema kuwa: "Wakati utawala huo ghasibu unapovurumisha mabomu ya fosforasi nyeupe na silaha hatari na za kisasa za kijeshi katika maeneo ya raia wasio na ulinzi, hili linamaanisha kuwa unatumia na kufanyia majaribio vikosi na uwezo wake wote".
Katika kujibu swali kuhusu misimamo dhaifu ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuhusiana na matukio ya Ghaza, Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar amesema: "Suala hili linapaswa kutathminiwa kwa mitazamo miwli. Kwa mtazamo wa kwanza wananchi wa madola ya Kiarabu na Kiislamu wanawaunga mkono watu wa Gaza na kwa mtazamo wa pili viongozi wa nchi za Kiarabu walio chini ya satua na ushawishi wa kifikra, kisiasa, kitamaduni na kijamii wa Kimagharibi wametumbukia katika uhusiano wa kidhahiri na usio wa kidhahiri na Israel na madola ya Kimaghairbi na hasa Marekani".
"Kwa miaka mingi sasa Warepublican wa Marekani wanaomiliki viwanda vya silaha nzito wamelenga mali na maisha ya watu wa nchi nyinginezo duniani na wanataka kuzusha vita katika eneo la Mashariki ya Kati ili waweze kuongeza soko la silaha zao. Ni katika fremu hiyo ndio maana Wademocrat kwa kumiliki uwezo wa kiuchumi na kwa kutumia hadaa ya kisiasa wanataka kufungamanisha hatima ya nchi na mafuta ya petroli na kwa njia hiyo kuangamiza uchumi wa nchi za ulimwengu wa tatu", amesema afisa huyo wa utamaduni wa Iran.
Hujjatul Islam Walmuslimin Moustafa Ranjbar amedokeza kuwa, miongoni mwa viongozi wa nchi za Kiarabu na Waislamu wa kawaida kuna wale wanaowasaidia wanamapambano wa Gaza kwa siri na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na hawataki kutajwa.
Moustafa Ranjbar amemaliza kwa kusema kuwa: "Ni matumaini yangu kuwa vita hivi vitamalizika kwa ushindi wa watu wa Gaza na wanamapambano wa Hamas". 348296