Ali Juma, Mufti wa Misri amewataka Waislamu kuwapa zaka zao wananchi wa Gaza ambao wamekuwa chini ya mashambulio makali na ya kinyama ya Wazayuni. Amesisitiza kwamba, wakazi wa Ukanda wa Gaza hivi sasa wako katika mstari wa mbele wa watu wanaopaswa kupewa zaka.
Mufti huyo ametoa taarifa akisema kuwa, kupewa zaka watu hao, kuwasaidia wawafukuze maadui wa Kizayuni kutoka kwenye ardhi yao na kusaidia kunusuru maisha yao ni katika njia za kufanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Mufti Ali Juma amesema, Uislamu haujabana jihadi katika kuwatetea Waislamu kwa silaha tu bali kuna jihadi ambayo hutekelezwa kupitia maneno na mali. Amesisitiza kwamba, Uislamu unachukulia juhudi au jambo lolote lile lililo katika uwezo wa Muislamu kwa ajili ya kuulinda Uislamu na Waislamu kuwa ni jihadi.
Mufti wa Misri amesema, jihadi inaweza kutimia kwa kutolewa misaada kama vile chakula, madawa na zaka kwa watu wanaopigana kwa jili ya Mwenyezi Mungu. Vilevile amezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kutoa zaka zao kwa Wapalestina hao wanaokabiliwa na hujuma ya kinyama ya Wazayuni pamoja na wakimbizi wa Kipalestina na vilevile kushiriki vilivyo katika ujenzi mpya na ukarabati wa Ukanda wa Gaza. 350140