Haniya amesema katika ujumbe huo kwamba matukio ya Gaza ni neema ya Mwenyezi Mungu na kwamba wanamapambano wa Kipalestina wameulazimisha utawala unaoikalia Quds kwa mabavu kuondoka katika ardhi ya Gaza kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.
Ameongeza kuwa Israel haikufikia hata moja kati ya malengo yake na kwamba wapiganaji wa Hamas wameweza kukwamisha matakwa ya kujipanua ya utawala huo.
Ismail Haniya amewaambia wananchi wa Palestina katika ujumbe huo uliorushwa hewani na televisheni ya Quds kwamba taifa la Palestina liko katika kipindi cha ushindi wa kistratijia na zinapaswa kufanyika juhudi za kukomboa Quds na msikiti wa al Aqsa.
Haniya ametoa wito wa kupelekwa misaada ya dharura kwa majeruhi na watu walioathirika na mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza na akasisitiza kwamba serikali ya Hamas itatoa misaada kwa familia ambazo nyumba na makazi yao yameharibiwa katika mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina ametoa wito wa kutumwa kamati ya kimataifa ya kuchumguza jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuwafikisha viongozi wa utawala huo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Ismail Haniya amesema kuwa Hamas imechukua uamuzi kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza ili adui Mzayuni aondoe askari wake katika eneo hilo na kwamba uamuzi huo wa busara unaonyesha jinsi harakati hiyo ya Kiislamu inavyojali maslahi ya wananchi.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imetangaza kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza na kuupa utawala ghasibu wa Israel muhula wa wiki moja kuondoa majeshi yake kikamilifu katika eneo hilo na kufungua vituo vya mpakani kwa ajili ya kuruhusu misaada ya kibinadamu. 350591