IQNA

Makanisa ya Uingereza yataka kutangazwa vipindi vya misaada kwa watu wa Gaza katika televisheni ya BBC

13:50 - January 27, 2009
Habari ID: 1736442
Rowan Williams, Askofu Mkuu wa Kanisa la Canterbury la nchini Uingereza amezitaka kanali zote za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kutangaza vipindi vya misaada kwa ajili ya wakazi wa Ukanda wa Gaza ambao wameathirika kutokana na mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel.
Askofu Williams amesema kwamba, kutangazwa vipindi na matangazo hayo ya misaada hakuna uhusiano wowote na siasa za kutopendelea upande wowote za televisheni hiyo na kwamba hiyo ni hatua tu ya kibinadamu inayopaswa kutekelezwa kwa haraka kwa ajili ya kuwasaidia watu hao wasio na ulinzi.
Dr John Sentamu, Askofu Mkuu wa York nchini Uingereza pia ametaka kutangazwa vipindi hivyo katika vyombo vyote vya habari vya nchi hiyo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukanda wa Gaza na pia ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na utawala wa Israel.
Kuhusiana na suala hilo, wabunge 51 wa Uingereza pia wamesema kuwa watawasilisha mswaada katika bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuvishawishi vyombo vya habari vya nchi hiyo kutangaza vipindi vinavyohusiana na umuhimu wa kutolewa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Televisheni ya satalaiti ya al-Jazeera na nyingine za Magharibi zimeanza kutangaza vipindi kama hivyo kwa ajili ya watu wa Gaza.
Ijumaa iliyopita, Mark Thompson, Mkuu wa BBC alidai kwamba vipindi hivyo vitaathiri vibaya fikra za waliowengi kuhusiana na imani waliyonayo kwa shirika hilo la utangazaji na hivyo kupoteza kile alichodai kuwa ni imani yao ya shirika hilo kutopendelea upande wowote katika shughuli zake za utangazaji. 354310
captcha