IQNA

Malaysia yapendekeza tamasha ya filamu ya nchi za Kiislamu

12:10 - January 29, 2009
Habari ID: 1737380
Waziri wa Habari wa Malaysia amependekeza kuanzishwa maonyesho ya filamu ya nchi za Kiislamu.
Akizungmza katika kikao cha mawaziri wa habari wa nchi za Kiislamu kinachofanyika Rabat, Ahmad Shabri Jak ametoa pendekezo hilo kwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC. Amesema, kunapaswa kuwepo tamasha ya sinema kama ile a Cannes na Berlin na kupendekeza kuwa jina la tamasha hiyo liwe 'Tamasha ya Filamu ya OIC' ili Wazalishaji filamu waweze kutumia jukwaa hilo kuwasilisha kazi zao na kubadilishana mawazo.
Amesema, kanali za televisheni za nchi za OIC zinapaswa kuonyesha filamu zinazozalishwa na nchi wanachama ili kukuza utamaduni wa Kiislamu na kuleta umoja na udugu baina ya nchi wanachama.
Ahmad Shabri Jak ametaka nchi za Kiislamu kukabiliana na vyombo vya habari na mawasiliano ambavyo vinachafua sura ya Uislamu. Aidha ametaka vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu kusambaza habari na taswira sahihi kuhusu matukio ya ulimwengu wa Kiislamu ili kuondoa taswira potofu zilizopo kuhusu Waislamu.
Waziri wa Habari wa Malaysia amesema kuwa kuna haja ya kubuniwa kanali ya habari ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na kuongeza kwamba, 'kuanzishwa kanali ya kimataifa ya kutangaza habari za nchi za Kiislamu ni jambo litakalosaidia kufikiwa lengo hilo'.
Akiashiria kadhia ya Gaza na jinai za Israel katika eneo hilo amesema kuwa, bunge la Malaysia limeutaka Umoja wa Mataifa kuanzisha mahakama ya jinai za kivita za utawala wa Kizayuni huko Gaza. Amesema, ili kufanikisha suala hilo, OIC inapaswa kuwa na mikakati zaidi ili hatimaye watawala wa Israel wafikishwe kizimbani. 355707
captcha