IQNA

Mkutano wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu nchini Iraq

11:01 - January 31, 2009
Habari ID: 1737741
Mkutano wa kuchunguza njia za kuwakurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu ulifunguliwa jana katika Kitengo cha Fiqhi cha Chuo Kikuu cha Kufa nchini Iraq.
Mkutano huo unasimamiwa na Abdulhadi Muhammad Taqi al Hakiim ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa fiqhi wa madhehebu ya Shia akishirikiana na maulamaa wa Kishia na Kisuni.
Sabah Anuz, Mkuu wa Kitengo cha Fiqhi cha Chuo Kikuu cha Kufa amesema kuwa, mkutano huo utajadili njia za kuimarisha maelewano kati ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu, kukabiliana na njama za maadui za kuzusha hitilafu na migawanyiko ya kimadhehebu na kikabila na kutoa majibu kwa uzushi unaotolewa kuhusu ibada na ada za kidini za Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Ameongeza kuwa mkutano huo pia utachunguza matamshi ya kichochezi yaliyotolewa miezi kadhaa iliyopita na Sheikh Yusuf Kardhawi ambaye ni Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu akidai kwamba Mashia wanafanya juhudi za kusambaza madhehebu hiyo katika jamii za Kisuni kwa kutumia fedha.
Abdulhadi Muhammad Taqi al Hakim ambaye alihutubia mkutano huo, amesema kuwa kizazi kipya cha Waislamu kinapaswa kutupilia mbali hitilafu na migawanyiko ya kimadhehebu, kuzidisha juhudi za kuimarisha umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu na kukabiliana na changamoto zinazoikabili dini yao.
Amesema kuwa Sheikh Yusuf Kardhawi ni miongoni mwa shakhsia wakubwa wa Kiislamu lakini inasikitisha kwamba matamshi yake ya kichochezi dhidi ya Waislamu wa Kishia yamezusha ufa na hitilafu zaidi kati ya Waislamu. 356394
captcha