Kituo cha intaneti cha Islam Online kimeripoti kuwa kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo, Waziri wa Ulinzi wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni Benyamin bin Eliezer, Mkuu wa Shirika la Usalama wa Ndani, kamanda wa jeshi la Israel, kamanda wa kikosi cha jeshi la anga la utawala huo, Mkuu wa Usalama wa Taifa na Mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo wamepatikana na makosa ya kutenda jinai za kivita dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mwaka 2002.
Taarifa ya Mahakama ya Taifa ya Uhispania imesema kuwa viongozi hao wa utawala wa Israel walituhumiwa kwamba tarehe 22 Julai mwaka 2002 walirusha bomu lenye uzito wa tani moja katika eneo la al Durj karibu na Ukanda wa Gaza kwa kutumia ndege aina F-16 kwa shabaha ya kumuua Salah Shahada ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya Hamas. Bomu hilo lilimuua shahidi mwanaharakati huo pamoja na raia 14 wakiwemo watoto tisa na wanawake 3 na kujeruhi vibaya wengine 150.
Mahakama ya Taifa ya Uhispania ambayo ndiyo chombo cha juu kabisa cha sheria nchini humo, iliitisha kikao cha mahakama na kutoa hukumu hiyo ya mwisho kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu cha Palestina dhidi ya viongozi saba wa ngazi za juu wa utawala wa Israel waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kutenda jinai za kivita Ukanda wa Gaza mwaka 2002.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kiongozi yeyote kati ya hao saba atakayeingia nchini Uhispania atatiwa nguvuni. 356385